Wanafunzi na wakufunzi wa Jundokan Karate Do Tanzania leo Jumapili, Julai 6, 2025, wameungana katika Gasshuku – yaani semina maalum ya karate – iliyofanyika kwa mafanikio makubwa katika viwanja vya Shule ya Sekondari Azania, jijini Dar es Salaam.
Neno “Gasshuku,” lenye asili ya Kijapani, linamaanisha “kambi ya pamoja ya mafunzo,” ambapo wakarateka wa viwango mbalimbali hukusanyika kwa siku nzima au zaidi ili kuimarisha ujuzi wao, kushiriki uzoefu, na kujifunza kwa pamoja katika roho ya karate-do.
Kuanzia saa tatu asubuhi hadi saa kumi jioni, washiriki walifundishwa na timu ya wakufunzi mahiri wakiongozwa na Sensei Yusuf Kimvuli, Naibu Mkurugenzi wa Ufundi wa Jundokan Karate Do Tanzania, akiwa na Sensei Maulid Pambwe, Sensei Dkt. Philip Swai, Sensei Bilal Mlenga na Sensei Wahid Aghful.
Washiriki kutoka mikoa mbalimbali nchini – wakiwemo kutoka Zanzibar, Morogoro, Dodoma, Mafinga na Moshi – walipitia vipindi mbalimbali vya mafunzo. Mafunzo yalianza kwa Jumbi Undo (mazoezi ya maandalizi ya mwili), yakafuatiwa na Kata (miondoko ya msingi ya karate) na kisha Bunkai, yaani maelezo ya nadharina ya vitendo ya hatua za Kata hizo.
Gasshuku hii ilionyesha sio tu umahiri wa wakufunzi na ukakamavu wa wanafunzi, bali pia mshikamano wa familia ya Jundokan nchini.