Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kwa kushirikiana na Kampuni ya SICPA Tanzania, inaendelea kuelimisha umma kuhusu nafasi ya teknolojia katika kulinda walaji, kuimarisha ulipaji wa kodi, na kulinda uchumi wa Taifa.
Hii ni sehemu ya jitihada za TRA za kuendeleza uwazi, uwajibikaji, na uchumi shirikishi unaowanufaisha wananchi wote.
Katika soko la leo linalobadilika kwa kasi, Watanzania wanakabiliwa na changamoto ya bidhaa bandia na biashara haramu zinazohatarisha afya na usalama wa walaji. Changamoto hizo pia zinadhoofisha ushindani wa haki na kuinyima Nchi mapato muhimu ya kodi ambayo hutumika kugharamia huduma za jamii.
Kutambua changamoto hizo kumeifanya TRA kuimarisha mikakati ya kutoa elimu kwa umma, ikiwa ni pamoja na kushiriki kwenye majukwaa muhimu ya kitaifa na kimataifa kama Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba), ili kuwasiliana moja kwa moja na wananchi na kuonesha jinsi mifumo ya kisasa ya kodi inavyowanufaisha.
Kupitia ushiriki huo, wananchi wananufaika kwa:
• Kupata uelewa wa moja kwa moja kuhusu jinsi Mfumo wa Stempu za Kodi za Kielektroniki (ETS) unavyosaidia kutambua bidhaa halali na kulinda walaji dhidi ya bidhaa hatarishi.
• Kujifunza kwa vitendo kutumia programu ya Hakiki Stempu, inayowawezesha walaji kuthibitisha uhalali wa bidhaa kabla ya kununua. Programu hiyo rahisi inamwezesha kila mwananchi aliye na simu janja kuhakikisha bidhaa kama vile vinywaji baridi, vileo, na sigara ni halali na salama.
• Kupata maarifa kuhusu uhusiano wa moja kwa moja kati ya ulipaji wa kodi na maendeleo ya Taifa, na kuelewa jinsi bidhaa halali na kodi inayolipwa inavyochangia ujenzi wa shule, hospitali, barabara na huduma nyingine muhimu kwa maisha bora ya wananchi.
Akizungumzia umuhimu wa jitihada hizo, Meneja wa Mradi wa ETS kutoka TRA, Bw. Abyud Tweve alisema, “Teknolojia hizo hazijaletwa tu kwa ajili ya kuboresha ulipaji wa kodi, bali pia kwa ajili ya kuwawezesha na kulinda afya ya wananchi. Kushiriki kwenye matukio ya kitaifa kama Sabasaba kunatupa nafasi muhimu ya kuzungumza moja kwa moja na wananchi na kuwaonyesha jinsi wanavyoweza kushiriki katika kulinda biashara za haki na kusaidia maendeleo ya Taifa.”
Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa SICPA Tanzania, Bw. Alfred Mapunda aliongeza, “Teknolojia inapoambatana na uelewa wa jamii inakuwa nguvu kubwa ya kuleta maendeleo. Ushirikiano wetu na TRA unaonyesha dhamira ya kuhakikisha kila Mtanzania anaelewa na kutumia teknolojia hizi kulinda haki zao, kusaidia uwazi, na kujenga soko lenye usawa.”
Ushiriki wa TRA katika majukwaa kama Sabasaba unaakisi azma yake ya kufanya kazi kwa karibu na wananchi katika kujenga utamaduni wa ulipaji kodi na uwajibikaji wa pamoja.
TRA inawahimiza Watanzania wote kukumbatia teknolojia hizo, kuendelea kujielimisha, na kushiriki kikamilifu katika kulinda maslahi yao na kuchangia katika uchumi thabiti na endelevu.
Karibu tutembelee katika Banda letu na pakua programu ya Hakiki Stempu kupitia App store.