Jukwaa la Watendaji Wakuu wa Sekta Binafsi Tanzania (CEOrt Roundtable) limeadhimisha miaka 25 tangu kuanzishwa kwake kwa kuandaa tukio maalum la mbio za ‘CEOrt Legacy Walk’, zilizofanyika jijini Dar es Salaam.
Maadhimisho haya ya robo karne yamelenga kuenzi mafanikio ya uongozi, ushirikiano na mchango wa sekta binafsi katika maendeleo ya taifa, sambamba na kuhamasisha umuhimu wa afya kwa viongozi wa taasisi na jamii kwa ujumla.
Akizungumza katika tukio hilo, Mwenyekiti wa CEOrt, Bw. David Tarimo, alisema kuwa jukwaa hilo limekuwa mstari wa mbele katika kukuza uongozi wa maadili, utetezi wa maslahi ya sekta binafsi, na kuimarisha majadiliano kati ya sekta binafsi na Serikali — kama mhimili muhimu wa maendeleo ya taifa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa CEOrt, Bi. Santina Benson, alieleza kuwa kwa kipindi cha miaka 25, jukwaa hilo limewezesha mageuzi katika maeneo muhimu yanayochochea mabadiliko ya kiuchumi kupitia ushiriki wa sekta binafsi.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania, Bw. Philip Besiimire, alisema kampuni hiyo inajivunia kuwa sehemu ya safari ya mafanikio ya CEOrt. Alisisitiza kuwa Vodacom, ambayo pia inaadhimisha miaka 25 ya kutoa huduma za mawasiliano nchini, imesaidia kuiunganisha Tanzania na kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa taifa kupitia ushirikiano na CEOrt.