Na Said Mwishehe,Michuzi Blog
BARAZA la Masoko ya Mitaji (CMT) ambayo ni taasisi ya haki ya madai kwenye mfumo wa kifedha nchini Tanzania limetoa rai kwa Watanzania kuendelea kupata elimu ya fedha ambayo itasaidia pia kujua sehemu gani sahihi ya kuwekeza katika masoko ya Miraji na dhamana.
Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa semina kwa Waandishi wa habari, Msajili wa Baraza la Masoko ya Mitaji (CTM) Dk.Martin Kolikoli ametumia nafasi hiyo kusisitiza jamii kuwa na uelewa kuhusu elimu ya fedha.
“Baraza la Masoko ya Mitaji tulikuwa na semina na waandishi wa habari ambao kimsingi tumekubaliana kuna uhitaji mkubwa sana wa
Watanzania kuendelea kupata elimu ya fedha ambayo itasaidia sisi wote kuendelea kujua sehemu gani sahihi ya kuwekeza katika masoko ya mitaji na dhamana.
“Watanzania wanapaswa kujifunza kuhusu maeneo sahihi ya kuwekeza katika masoko ya mitaji ya dhamana, na pia kufahamu namna ya kutatua migogoro ya kifedha kwa kufuata mifumo rasmi. Elimu ya fedha ni msingi wa maamuzi bora ya kifedha,” amesema Dkt. Kolikoli.
Aidha amesema baraza hilo ni chombo maalum kilichoundwa kusikiliza na kutatua migogoro inayohusiana na sekta ya dhamana, hivyo ni vyema wananchi wakalitambua na kulitumia kwa manufaa yao.
“Sasa Baraza lipo, na ni sehemu rasmi ya kushughulikia migogoro ya sekta ya dhamana. Tunawakaribisha Watanzania kuendelea kujifunza kuhusu majukumu ya CMT na nafasi yake katika kuendeleza masoko ya mitaji hapa nchini,” ameongeza Dkt. Kolikoli.
Aidha, Dkt. Kolikoli amesisitiza kuwa huu ni wakati muafaka kwa Watanzania kuchangamkia fursa zilizopo katika uwekezaji, lakini akawaasa kuhakikisha wanapata elimu kutoka kwa watu na taasisi sahihi kabla ya kuwekeza.
Baraza la Masoko ya Mitaji linalenga kukuza maarifa ya kifedha kwa umma, kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu huduma zake, na kuanzisha mifumo ya kidijitali ili kurahisisha usajili na ufuatiliaji wa kesi mbalimbali za madai katika sekta ya dhamana.
Amefafanua kwamba wananchi wakiwa na elimu ya fedha hata wanapokuwa na migogoro basi watafahamu namna gani au njia gani watafuata kupata haki huku akisisitiza kwa sasa hivi baraza linasehemu maalum ya migogoro ya sekta hiyo ya mitaji na dhamana na baraza hilo linakuwa kamili ya mahakama kuu.
“Kwahiyo nafasi yetu tunaendelea kujifunza na pia tunawakaribisha watanzania wote kuja kwenye baraza kupata elimu kujua baraza linamalengo gani na nafasi gani katika kuendeleza soko hili.”
Aidha Dk.Kolikoli amesema uwepo wa baraza hilo ni fursa ambayo watanzania wanatakiwa kuikimbilia kwasababu ukiangalia kila siku kuna bidhaa mpya inaingia kwenye soko.
Kuhusu kesi ambazo wamezipokea amesema hadi sasa wamepokea kesi moja ambayo wameshaitolea uamuzi lakini ameeleza kwamba soko liko salama ndio maana hali iko shwari
Akizungumzia wajibu wao amesema wanatoa maamuzi kwa haraka,yasiyo na upendeleo na yanayozingatia sheria juu ya migogoro ya masoko ya mitaji.Iwe ni mvutano na mamlaka ya usimamizi au suala lolote kuhusu utendaji usioridhisha wa masoko.“Tupo kukusikiliza ,kukuongoza na kuzingatia weledi katika utekelezaji wa majukumu yetu kisheria”
