
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, ameonyesha kuridhishwa na utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji unaojengwa kwa gharama ya Dola za Kimarekani milioni 53, ambao hadi sasa umefikia asilimia 68 ya ujenzi wake.
Akizungumza na wananchi mara baada ya kukagua maendeleo ya mradi huo uliopo juu ya milima ya Mtaa wa Kagera, katika Halmashauri ya Manispaa ya Geita, Waziri Aweso amesema dhamira ya serikali ni kuhakikisha kuwa wakazi wa mji wa Geita wanapata huduma ya maji ya uhakika na ya kutosha.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, aliwashukuru wananchi kwa ushirikiano waliouonesha wakati maeneo yao yalipopitiwa na ujenzi wa miundombinu ya mradi huo.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mjini Geita (GEUWASA), Mhandisi Frank Changawa, alieleza kuwa mradi huo unatekelezwa kwa kasi nzuri, huku akifafanua kuwa maeneo mengi ya mji huo yatanufaika na huduma ya maji mara baada ya kukamilika kwa ujenzi.