Na Mwandishi wetu, NCAA Dodoma.
Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Dkt. Pindi Chana (Mb) ametoa wito kwa watanzania wa kada mbalimbali kutembelea maonesho ya Nanenane yanayofanyika kitaifa viwanja vya nzuguni Jijini Dodoma pamoja na maeneo mengine nchini ili waweze kupata elimu ya vivutio vya utalii vilivyopo katika maeneo mbalimbali yaliyohifadhiwa.
Waziri Chana ametoa maelezo hayo akizungumza na waandishi wa habari alipotembelea banda la Wizara ya Maliasili na Utalii katika maonesho ya wakulima nanenane yanayofanyika kitaifa viwanja vya Nzughuni Dodoma ambapo wizara ya Maliasili na Utalii na taasisi zake inashiriki maonesho hayo kwa lengo la kutangaza vivutio vya utalii, kutoa elimu ya shughuli za uhifadhi, fursa za uwekezaji na maendeleo ya jamii.
“Natoa wito kwa watanzania kutembelea maonesho ya nanenane katika kanda zote yanapofanyika ili wapate elimu ya vivutio vya utalii tulivyonavyo, fursa za uwekezaji, elimu ya uhifadhi, na ufugaji nyuki. Wizara inaendelea kuongeza mazao mbalimbali ya utalii ikiwemo utalii wa vyakula na utalii wa kilimo kwa kuwa maonesho haya yamefunganisha sekta mbalimbali ili tuendelee kutangaza nchi yetu na kupata maendeleo kwa pamoja” aliongeza Balozi Chana.
Mamlaka ya Hifadhi ya eneo la Ngorongoro (NCAA) inashiriki maonesho hayo kwa lengo la kutangaza vivutio vya utalii kama vile Kreta za Ngorongoro, empakai, Olmoti, mlima Lolmalasin ambao ni wa tatu kwa urefu Tanzania, maporomoko ya maji endoro sambamba na mapango ya Tembo.
Vivutio vingine vinavyotangazwa katika maonesho hayo ni pamoja na Utalii wa malikale kama Makumbusho ya Olduvai, Nyayo za Laetoli, mchanga unaohama, utalii wa anga katika Kimondo cha Mbozi na Mapango ya Amboni Tanga yenye historia mbalimbali ikiwemo harakati za kudai uhuru wa Tanzania bara urithi na utamaduni wa makabila na watu wa Tanga.
Wageni wanatakaotembelea banda la Wizara ya Maliasili na Utalii pia watapata fursa ya kushuhudia mubashara vivutio vya utalii vilivyopo Ngorongoro kupitia “TV Screen” kubwa iliyofungwa kwenye banda hilo.
Kauli mbiu ya maonesho ya nanenane kwa mwaka 2025 ni “Chagua viongozi bora kwa maendeleo endelevu ya kilimo, mifugo na Uvuvi”