Baadhi ya wakulima wa Tumbaku katika kijiji cha Suluti Wilayani Namtumbo,wakisubiri kuuza tumbaku kwenye mnada wa mwisho wa zao hilo jana.
Na Mwandishi Wetu,Namtumbo
BAADHI wakulima wa Tumbaku katika kijiji cha Suluti Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma,wamefurahia kuongezeka kwa wanunuzi wa zao hilo ambalo kwa muda mrefu halikuwa na soko la uhakika.
Aidha,wameiomba Serikali kupitia wizara ya kilimo na ushirika, kuwatafutia masoko ya uhakika ya kuuza Tumbaku wanayolima ili waweze kurudisha gharama za uzalishaji na kujikomba na umaskini kupitia zao hilo.
Wakizungumza kwenye mnada wa mwisho wa zao hilo uliofanyika katika ghala la Chama cha Msingi Suluti wamesema,miaka ya nyuma wananchi waliokuwa wanalima zao hilo walikuwa wachache kwa sababu walikata tamaa baada ya kutokuwepo kwa soko la uhakika.
Said Mwichande alisema,baada ya kuongezeka kwa makampuni mbalimbali yanayonunua Tumbaku wakulima wengi wamehamasika kulima zao hilo kutokana na uwepo wa soko la uhakika na ameipongeza Serikali kwa usimamizi nzuri wa soko la Tumbaku kupitia mfumo wa stkabadhi ghalani.
“Baada ya kuongezeka kwa wanunuzi wa Tumbaku tunayolima,sisi wakulima tumehamasika na kupata nguvu kubwa ya kuzalisha Tumbaku,hata hivyo tunaiomba sana Serikali iendelee kututafutia masoko ili tuweze kupanua mashamba yetu”alisema Mwichande.
Mkulima Shafi Mbonde,ameishukuru Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan,kwa kuwapa mbolea za ruzuku zilizoongeza uzalishaji wa Tumbaku.
Alisema,awali mbolea zinazotumika kwenye uzalishaji wa Tumbaku ziliuzwa kati ya Sh.150,000 hadi 170,000 mfuko mmoja wa kilo 50 lakini katika msimu wa kilimo 2024/2025 wamenunua kwa kati ya Sh.52,000 hadi 54,000 hivyo kuhamasisha watu wengi wakiwemo vijana kuanza kulima zao hilo.
“mwaka huu tumenunua mbolea aina ya SA inayotumika kwenye zao la Tumbaku kwa bei ndogo sana ikilinganisha na miaka ya iliyopita,hivyo tunaiomba sana Serikali yetu mpango wa mbolea za ruzuku uwe endelevu ili tuweze kuzalisha kwa wingi”alisema Mbonde.
Mwenyekiti wa Chama cha msingi Suluti Amcos Athuman Mgahama alisema,mbolea za ruzuku zimesaidia sana kuongeza uzalishaji mashambani na wakulima kujipatia kipato hali iliyowezesha kupungua kwa umaskini katika kijiji hicho.

Baadhi ya wakulima wa Tumbaku katika kijiji cha Suluti Wilayani Namtumbo,wakisubiri kuuza tumbaku kwenye mnada wa mwisho wa zao hilo jana.

Sehemu ya shehena ya Tumbaku iliyohifadhiwa kwenye ghala la Chama cha Msingi cha Ushirika Suluti Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma kwa ajili ya kuuzwa kwa mnada.

Mwenyekiti wa Chama cha msingi cha Ushirika Suluti Amcos Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma Athuman Mhagama kushoto,akizungumza na baadhi ya wakulima walioleta Tumbaku kwenye ghala la Chama hicho kabla ya kuuzwa kwa njia ya mnada.