Othman Masoud , kuwa mgombea urais wa Zanzibar.
Luhaga Mpina Mgombea nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
………….
MKOA WA DAR ES SALAAM
Mkutano Mkuu wa Taifa wa Chama cha ACT wazalendo umewachagua Mhe. Othman Masoud , kuwa mgombea urais wa Zanzibar na ndugu Luhaga Mpina kugombea nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania watakaopeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Aidha ndugu Fatma Abdlhabib Fereji ameteuliwa kuwa Mgombea mwenza wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuthibitishwa bila kupingwa na wajumbe wote wa mkutano wa Halmashauri Kuu ya chama hicho iliyoketi katika ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es Salaama Agosti sita mwaka huu 2025.
Akitangaza matokeo baada yauchaguzi mbele ya mkutano mkuu huo, Mwenyekiti wa Kamati maalum ya Uchaguzi ya Chama hicho Mbarala Maharagande, amesema kwamba kura zote zilizopigwa kwa Mhe. Othman zilikuwa 610 ambapo amepata jumla ya kura 606 sawa na asilimia 99.5 wakati kura tatu zilisema hapana na kura moja iliharibika.
Kwa upande wa mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndugu Luhanga Mpina aliyetokea chama cha Mapinduzi hivi karibuni na kuhamia ACT amepata kura 559 sawa na asilimia 93 ya jumla ya kura zote 610 huku kura halili zikiwa ni jumla ya 605 na kumbwaga mpizani wake Ndugu Aaron Kalikawe aliyepata kura 46 tu sawa na asilimia 7.7 wakati kura tatu ziliharibika .
Aidha ndugu Mpina baada ya kuchaguliwa alimpendekeza ndugu Fatma Abdulihabib Fereji chini ya Ibara ya 68 kifungu kidogo cha kwanza ( A), cha katitba ya ACT Wazalendo kuwa mgombea mwenza na kulipeleka jina hilo mbele ya Halmashauri Kuu ya chama hicho ambapo alipitishwa bila kupingwa .
Akitoa salamu za shukrani baada ya matokeo hayo mgombea urais wa Zanzibar ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa Chama hicho Mhe. Othman Masoud Othman amesema kwamba chama hicho kimempa heshima kubwa kusimamia matarajio ya zanzibari na watanzania kwa jumla na kwamba atafanya juhudi kwa dhati kutimiza matarajio ya wananchi.
Amesema kwamba dhamira ya chama hicho ni kuwapambania watanzania wote kuondokana na matatizo ya kiuchumi na kijamii yaliyopo ambapo Tanzania licha ya utajiri mkubwa wa rasilimali kama vile ardhi, mito wanyama, maliasli na madini iliyonao lakini kutokana na uongozi mbaya wananchi wake wanaendelea kugubikwa na umasikini mkubwa .
Mhe. Othman amabye pia ni Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar ,amesema kwa utaratibu uliopo sasa wa kuendesha nchi chini ya utawala wa chama tawala kilichopo kamwe taifa la Tanzania haliwezi kuendelea kwa kuwa rasilimali za nchi zimegeuzwa keki ambayo watu wanaendelea kugawana na viongozi kushindwa kuwajibika mbele ya wananchi waliowachagua.
Amesema kwamba dhamira ya chama hicho ni kuleta mageuzi ya kweli ya kiuongozi na kuwajibikaji na kisiasa na kwamba ni muhimu wananchi wote kukiunga mkono chama hicho ili kiwezeze kushinda na kuleta mabadiliko ya matumaini ya kimaendeleo ya kiuchumi na kisiasa wanayoyataka wananchi wa Tanzania hivi sasa.
Mhe. Othman amewashukuru wajumbe wa mkutano huo na chama hicho kwa jumla na kuwataka watanzania kwamba lazima waelewe kuwa hii ndio nchi yao na kwamba ni muhimu kuungana pamoja katika kupambania mageuzi ya kweli kwa kulichukulia suala hilo la mageuzi kwa umakini mkubwa.
Kwa upande wake Mgombea wa Chama hicho nafasi ya urais wa Jamhuri yan Muungano wa Tanzania Luhanga , ameahidi kwamba anatahakikisha anashirikiana na viongozi wenzake wa ACT na wananchi kuifikia mikoa yote ya Tanzania ili kusaka kura kuanzia saa sita usiku tarehe ya kampeni iliyopangwa mwezi huu kama ilivyoelekezwa na Tume huru ya Uchaguzi ya Tanzania.
Amewasifu pamoja na kuwashukuru wajumbe na wananchama wa chama hicho kwa kumpokea na kumpa imani kumbwa na kuahidi kwamba atajitahidi katika kuhakikisha kwamba matumaini mapya ya kuleta mageuzi waliyonayo watanzania kwa pamoja wanayafikia kwenye uchaguzi mkuu ujao na kwamba alichelewa sana kujiunga na chama hicho kinachofuata demokrasia ya kweli na uwazi katika taratibu zake mbali mbali.
Amesema kwamba hivi sasa kazi yake kubwa ni kuwapelekea ujumbe wa kuleta mageuzi watanzania wote popote walipo kuhakikisha kwa pamoja wanajiandaa na maeguzi katika kuipata Tanzania mpya chini ya chama cha ACT wazalendo.
Kwa upande wake mgombe mwenza wa Chama hicho Fatma Ferereji ameahidi kuiitendea haki imani aliyopewa na chama hicho na watanzania kwa jumla katika kuhakikisha kwamba dhima na dhamana aliyopewa anaitimiza vyema kama yalivyo matarajio ya watanzania wote.
Amesema kwamba hivi sasa juhudi kubwa zitaelekezwa kutafuta kura zaidi za watanzania na kwamba atajitahidi kutumia uwezo wake wote kurejesha shukrani na imani za wananchama wa chama hicho walizompa kwa kuhakikisha kwamba chama hicho kinapata ushindi.
Kikao cha Mkutano mkuu huo maalum wa uchaguzi huo pamoja na mambo mengine pia ulipitisha Ilani za uchaguzi ujao za chama hicho kwa bara na visiwani ulitanguliwa na vikao mbali mbali ikiwemo kamati ya uongozi, kamati ya maadili, kikao cha kamati kuu , halmashauri kuuu na hatimaye Mkutano mkuu uliowapata wagombea Urais.