

Kundi la waasi wa M23 linalodhibiti maeneo ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) limepinga tuhuma za kuhusika katika mauaji ya raia jimboni Kivu Kusini na madai ya kuajiri askari watoto.
Kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la Uingereza-BBC, Msemaji wa M23, Willy Ngoma amesema kuwa kundi hilo halina nia ya kuwalenga raia. “Hatuui raia … Tunawezaje kuua raia ambao tunapaswa kuwalinda? Hatuwezi hata kuua kuku wao… tunaheshimu raia,” amesema Ngoma.
Hivi karibuni, Jeshi la DRC lililishutumu M23 kwa mauaji hayo, likiungwa mkono na ripoti ya ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa (UN) iliyoeleza kuwa lina ushahidi wa moja kwa moja kwamba zaidi ya raia 300 waliuawa mwezi uliopita na waasi hao wanaodaiwa kuungwa mkono na Rwanda.

Ngoma amesisitiza kuwa Umoja wa Mataifa haujafika kujionea hali halisi katika maeneo yanayodhibitiwa na M23, akiongeza kuwa taarifa wanazotoa mara nyingi zinatokana na maoni yenye upendeleo kutoka kwa serikali ya DRC.
Hata hivyo, wachambuzi wa siasa za kanda wanasema juhudi za upatanishi zinazofanywa na Marekani na Qatar bado zinakabiliwa na changamoto kubwa, na kufanikisha amani ya kudumu kunabaki kuwa jambo gumu kufikiwa.