
Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, leo Jumanne Agosti 12, 2025, imetupilia mbali maombi ya upande wa utetezi wa Tundu Lissu katika kesi ya marejeo (judicial review) iliyolenga kupinga matumizi ya mashahidi wa siri kama ilivyoombwa na upande wa Jamhuri.
Katika kesi ya msingi inayosikilizwa katika Mahakama ya Kisutu, Lissu anakabiliwa na shtaka la kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni. Jamhuri iliwasilisha ombi la kutumiwa kwa mashahidi wa siri, likidai usalama na masilahi ya mashahidi hao.
Uamuzi huo umetolewa na Jaji Elizabeth Mkwizu. Baada ya kusikiliza shauri hilo, mmoja wa mawakili wa Lissu, Dkt. Rugemeleza Nshala, aliwaambia wanahabari kuwa hawajaridhishwa na uamuzi huo, wakieleza kuwa hatua hiyo “inapoka haki ya mshtakiwa” kwa kumnyima fursa ya kuwajua na kuwakabili mashahidi dhidi yake.