DAR ES SALAAM: Klabu ya Simba imemtambulisha kiungo kiraka kutoka Guinea, Naby Camara, kama mchezaji huru kwa mkataba wa miaka miwili, utakaomuweka klabuni hapo hadi mwaka 2027.
Camara, mwenye umri wa miaka 23, anamudu kucheza kama kiungo wa kati na beki wa kushoto.
Nyota huyo atatumika kuongeza nguvu upande wa kushoto wa ulinzi, nafasi iliyoachwa wazi na Mohammed Hussein “Zimbwe Jr” ambaye amejiunga na Yanga.
Camara alianza soka lake katika akademi ya klabu ya Horoya AC, moja ya timu kubwa nchini humo, kabla ya kujiunga na CS Sfaxien ya Tunisia mwaka 2021. Akiwa na Sfaxien, alijipatia umaarufu kwa uwezo wake wa kupandisha mashambulizi na nidhamu ya kiufundi.
Msimu uliopita alikipiga katika Al-Waab Sporting Club ya Qatar, ambapo alionekana mara nyingi akitumika kama beki wa kushoto wa kuzuia na kushambulia.
Ujio wake unatarajiwa kuongeza ushindani ndani ya kikosi cha Simba, chini ya Kocha Fadlu Davids anayehitaji wachezaji wanaoweza kucheza nafasi zaidi ya moja uwanjani.
Mwisho
The post Naby Camara ni mali ya Simba tayari first appeared on SpotiLEO.