Na Mwandishi wetu– Mara
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Mara limetumia fursa ya Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa umeme, ili kuwaepusha na utegemezi wa kuni na mkaa ambao ni nishati zisizo safi na zenye athari kwa mazingira.
Akizungumza mbele ya Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2025, Afisa Uhusiano wa TANESCO Mkoa wa Mara, Bi. Joyce William, alisema nishati hiyo safi inajumuisha matumizi ya majiko ya umeme yanayotumia kiasi kidogo sana cha umeme tofauti na mtazamo wa wananchi wengi.
“Ndugu Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, majiko haya yanatumia umeme kidogo sana. Kwa mfano, kilo moja ya nyama inaweza kupikwa kwa kutumia unit 0.9 za umeme ambazo ni sawa na shilingi 321 pekee. Hii ni nafuu na inawasaidia wananchi kuondokana na hofu ya kutumia umeme kwa shughuli za kupikia,” alisema Bi. Joyce.
Aidha, alibainisha kuwa TANESCO imejipanga kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye amekuwa mstari wa mbele kusisitiza matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kulinda mazingira na kupunguza gharama za maisha kwa wananchi.
Kwa upande wake, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Ndg. Ismail Ali Ussi, amelipongeza Shirika la Umeme Tanzania kwa ubunifu na juhudi zake za kuhamasisha wananchi kubadili mtazamo na kuachana na matumizi ya kuni na mkaa, na badala yake kuhamia kwenye nishati safi na salama kwa afya na mazingira.