Na Meleka Kulwa – Dodoma
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko, ametoa onyo kali kwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kufuatia kusuasua kwa Mradi wa Ujenzi wa Njia ya Kusafirisha Umeme wa Msongo wa Kilovoti 400 kutoka Chalinze hadi Dodoma.
Akizungumza alipokuwa akitembelea mradi huo leo Agosti 20, 2025, Dkt. Biteko alisema kuwa mradi huo umefikia asilimia 24 pekee badala ya asilimia 31 iliyopangwa tangu ulipozinduliwa.
Amesema kusuasua kwa mradi huo kunahatarisha mpango wa taifa wa kuunganisha umeme kutoka Bwawa la Kufua Umeme la Mwalimu Julius Nyerere kwenda mikoa mbalimbali nchini.
“Tusizuie miradi hii, kwa sababu viwanda na wananchi wanahitaji umeme wa uhakika. Tunaongeza vyanzo vingine vya umeme kwenye gridi ya taifa ili kuhakikisha nchi inakuwa na umeme wa kutosha kwa maendeleo ya viwanda na huduma za kijamii,” amesisitiza Dkt. Biteko.
Aidha, Naibu Waziri Mkuu amewaomba wananchi wa Manchali na Dodoma kwa ujumla kushirikiana na serikali na kujitokeza kwa wingi katika mikutano ya kampeni mwaka huu, akisisitiza umuhimu wa kuchagua viongozi wanaoeleza yale waliyotekeleza badala ya matamanio pekee.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Bi. Rosemary Senyamule, amesisitiza kuwa serikali ya mkoa huo itahakikisha mradi huo unasimamiwa kikamilifu hadi kukamilika.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO, Lazaro Twange, ameahidi kushughulikia mapungufu yote yaliyochangia kuchelewesha utekelezaji wa mradi huo.
Vilevile, baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Manchali, ambapo mradi huo unatekelezwa, wametoa maoni yao wakiiomba serikali kuharakisha utekelezaji wake ili waweze kupata huduma ya umeme mapema.
Nasson Tunjeletona, mkazi wa Manchali, amesema mradi wa Chalinze–Dodoma unatajwa kuwa kiunganishi muhimu katika usafirishaji wa umeme wa uhakika kutoka Bwawa la Nyerere, hatua inayotarajiwa kuchochea maendeleo ya viwanda na uchumi wa taifa.