
Dunia imepoteza alama ya haki yenye huruma. Jaji Frank Caprio, ambaye alijipatia umaarufu duniani kupitia kipindi chake cha televisheni Caught in Providence, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 88 kutokana na saratani ya kongosho.
Caprio hakutambulika tu kama jaji, bali kama sauti ya upendo na ubinadamu katika mfumo wa sheria. Kupitia mtindo wake wa kuendesha kesi, alionesha kwamba mahakama inaweza kuwa mahali pa haki na huruma kwa wakati mmoja.
Video zake zilizosambaa mitandaoni ziliwaonesha maelfu jinsi gani alivyowapa nafasi watu kueleza hali zao kabla ya kutoa hukumu.
Mfano maarufu ni pale alipomruhusu mzee mwenye umri wa miaka 96 kuondoka bila adhabu ya faini ya mwendo kasi. Mzee huyo alimweleza kuwa alikuwa akiharakisha kwa sababu ya kumpeleka mwanawe mgonjwa, mwenye ulemavu, hospitalini.
Caprio aliguswa sana na hadithi hiyo na badala ya kutoa adhabu kali, alimpongeza mzee huyo kwa kujitolea kwake kama baba. Tukio hilo lilienea duniani kote, likiwagusa watu kwa upole na utu aliouonesha.