Dar es Salaam, 22 Agosti 2025
Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa kushirikiana na Wizara za kisekta na wadau wa maendeleo imeandaa Maadhimisho ya Wiki ya Ustawi wa Jamii kwa mwaka 2025. Lengo kuu la maadhimisho haya ni kuimarisha na kuongeza ushiriki na uelewa wa wananchi kuhusu huduma za ustawi wa jamii, kuchochea utetezi wa haki za kijamii pamoja na kuendeleza jamii jumuishi inayothamini usawa na ustawi wa makundi yote hususan yale yaliyo katika mazingira hatarishi.
Kwa mwaka huu, maadhimisho haya yanafanyika nchi nzima ambapo Kitaifa yatafanyika jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 25 hadi 30 Agosti 2025 katika viwanja vya Chuo cha Ustawi wa Jamii Kijitonyama. Maadhimisho haya yanabeba hadhi ya kimataifa yakihusisha washiriki kutoka mataifa mbalimbali ikiwemo Kenya, Uganda, Zambia na Benin. Kaulimbiu ya mwaka huu ni “Pata Msaada wa Kisaikolojia; Imarisha Afya ya Akili” inayolenga kuhamasisha jamii kuwa na ujasiri wa kutafuta msaada wa kitaalam wanapokumbwa na changamoto za kisaikolojia. Mgeni rasmi katika maadhimisho haya anatarajiwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango.
Maadhimisho haya yamekusudia kutoa elimu na kujenga uelewa wa umma kuhusu huduma za ustawi wa jamii zinazopatikana nchini. Pia yanakusudia kuchochea matumizi na maboresho ya sera, sheria na miongozo ya huduma za ustawi wa jamii, kuhamasisha na kuimarisha ushirikiano kati ya wadau wa huduma hizi pamoja na kubadilishana uzoefu wa kitaifa na kimataifa katika utoaji wa huduma. Aidha, yanalenga kuwawezesha Maafisa Ustawi wa Jamii kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi na kuhimiza ulinzi na usalama wa makundi maalum ikiwemo wazee, watoto na watu wenye ulemavu.
Huduma mbalimbali zitakazotolewa katika maadhimisho haya ni pamoja na huduma za ustawi wa familia na watoto, elimu ya malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto, huduma kwa wazee na watu wenye ulemavu, huduma za marekebisho na ujenzi wa tabia, ushauri na unasihi wa kisaikolojia na kijamii, usajili wa vituo vya kulelea watoto mchana, makao ya watoto na nyumba salama. Pia kutakuwa na usuluhishi wa migogoro ya ndoa na familia, elimu ya malezi ya kambo na kuasili, huduma kwa manusura wa ukatili wa kijinsia na watoto, huduma za msaada wa kisheria, huduma za rufaa na upimaji wa afya kwa wazee pamoja na huduma za afya ya akili.
Aidha, wiki hii itaambatana na kampeni ya utoaji wa huduma za ustawi wa jamii katika halmashauri zote 184 nchini, utoaji wa elimu kwa umma kupitia vyombo vya habari, maonesho na utoaji wa huduma mbalimbali zikiwemo afya na msaada wa kisheria, kongamano la wamiliki wa makao ya watoto, nyumba salama na vituo vya kulelea watoto wadogo mchana pamoja na Mkutano Mkuu wa mwaka wa Maafisa Ustawi wa Jamii nchini utakaoshirikisha pia washiriki kutoka nchi rafiki.
Wizara inatoa wito kwa wananchi wote kujitokeza kwa wingi kushiriki katika maadhimisho haya ili kunufaika na huduma na elimu mbalimbali zitakazotolewa bure katika viwanja vya Chuo cha Ustawi wa Jamii Kijitonyama na katika maeneo mengine nchini. Tujitokeze kwa wingi kushiriki katika shughuli zote zitakazofanyika na hasa katika kilele cha maadhimisho haya tarehe 30 Agosti 2025 kwa mustakabali wa ustawi wa jamii yetu.
Imetolewa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mheshimiwa Dkt. Dorothy Gwajima.