

Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha limesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa mgombea udiwani kata ya Ngarenaro kupitia CCM, Abdulaziz Abubakari Chande maarufu kama “Dogo Janja”, alitumia silaha yake akijihami katika tukio lililosababisha kijana mmoja kujeruhiwa kwa risasi.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, SACP Justine Masejo, tukio hilo lilitokea Agosti 23 majira ya saa 5:30 usiku katika maeneo ya Sombetini, jijini Arusha, ambapo Bakari Halifa Daudi (18) alijeruhiwa kwa risasi mguuni.
“Uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa wakati Abdulaziz akishuka kwenye gari, alidai kuwa alitaka kuvamiwa na Bakari akiwa na mwenzake wakiwa na silaha za jadi. Hali hiyo ilisababisha mtuhumiwa kutumia silaha yake na kumpiga risasi Bakari,” imesema taarifa hiyo.
Kamanda Masejo amethibitisha kuwa polisi wamewakamata watu wawili kuhusiana na tukio hilo na kwamba uchunguzi zaidi unaendelea ili kubaini undani wa tukio na hatua zaidi za kisheria zitachukuliwa.
Bakari kwa sasa anaendelea kupatiwa matibabu kutokana na jeraha alilopata.