Baadhi ya Wanachama wa Chama cha Mapinduzi Wilayani Namtumbo Mkoani Ruvuma,wakimsindikiza Mgombea Ubunge wa Jimbo la Namtumbo kupitia Chama hicho Dkt Juma Homera anayepunga mkono, baada ya kuchukua fomu kwenye Ofisi za Tume Huru ya Uchaguzi(INEC)Picha na Muhidin Amri.
Na Mwandishi Maalum, Namtumbo
ALIYEWAHI kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Dkt Juma Zuber Homera,amechukua fomu ya kugombea Ubunge katika Jimbo la Namtumbo Mkoani Ruvuma kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi na kutangaza rasmi kuvunjwa kwa makundi yote yaliyokuwepo wakati wa mchakato wa kura za maoni ndani ya Chama hicho.
Akizungumza na mamia ya Wanachama na Wananchi wa Namtumbo kwenye ofisi za CCM Wilaya baada ya kukabidhiwa fomu na Msimamizi wa Tume huru ya Uchaguzi Jimbo la Namtumbo Jonah Katanga,Homera amewashukuru wajumbe wa kamati kuu wakiongozwa na Mwenyekiti Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumteua kugombe nafasi hiyo.
Alisema,dhamira yake kubwa ni kutaka kuwatumikia wananchi wa Namtumbo kwa kuwaletea maendeleo huku akiweka wazi kuwa hakuna chama cha kuletea maendeleo isipokuwa Chama cha Mapinduzi na kuwaomba wana CCM kumuamini kwani huu ni wakati sahihi wa yeye kuibadilisha wilaya hiyo.
Homera,amewahidi wana CCM na wananchi wa Namtumbo kwa ujumla kwamba atahakikisha anawatendea haki kwa kuleta maendeleo waliyosubiri kwa muda mrefu.
“ndugu zangu niwaambie tumeteseka sana,hali ya wilaya yetu ni mbaya kimaendeleo,nawahaidi nitakwenda kufanya kazi mliyonituma mimi kijana wenu,muhimu akikisheni mnanipigia kura nyingi siku ya tarehe 29 Oktoba mwaka huu”alisema Homera.
Homera alisema, kwa kuanzia tayari amezungumza na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya chakula(NFRA) kufungua kituo cha kuuza mahindi na imekubali kufungua kituo hicho ili wakulima wa Namtumbo wauze mahindi yao kwa Serikali.
Aidha,amewataka watumishi wa Serikali wilayani humo wanaoshindwa kwenda na kasi ya Serikali ya awamu ya sita wajiandae kuondoka haraka katika na kwenda maeneo mengine ya kufanya kazi ya utumishi badala ya kuendelea kuwa Namtumbo.
“Kwa kuanza nimeshazungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya yetu ya Namtumbo nimemwambia atafute eneo kubwa kwa ajili ya kujenga stendi mpya na soko la kisasa,ile siyo stendi katika haistahili kuwepo katika mji wetu wa Namtumbo”alisema.
Homera,amewaomba wanachama waliojitokeza kwenye mchakato wa kura za maoni ndani ya CCM kuungana naye kupigania kura za Chama cha Mapinduzi katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika tarehe 29 Oktoba mwaka huu.
“Suala la kura za maoni ndani ya chama limekwisha,sisi sasa wote ni Chama cha Mapinduzi,tofauti zilizokuwepo wakati wa kura za maoni zimekwisha tufanye kazi ya Chama chetu”alisisitiza Homera
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Zuberi Lihuwi,amewashukuru wajumbe wa kamati ya Siasa Wilaya kwa kazi nzuri waliyofanya kupitishajina la mwanachama mwenye sifa atakayepeperusha bendera ya Chama hicho kwa nafasi ya Ubunge kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwezi Oktoba.
Amempongeza Homera,kwa kuaminiwa na kukubalika na Chama hicho kwani kati ya kura 13,000 zilizopigwa na wajumbe Homera alipata kura 11,836 na kuwashinda wanachama wengine wanne waliochukua fomu ya kuomba ridhaa ya Chama cha Mapinduzi.
Lihuwi,amewaomba wana CCM kuwa kitu kimoja,kuvunja makundi yaliyokuwepo wakati wa kura za maoni na kuunganisha kura zao kwa Homera ili aweze kupata ushindi wa kishindo badala ya kuendelea na makundi yanayoweza kukiathiri Chama chao.
Awali Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Namtumbo Jonah Katanga alisema,hadi sasa jumla ya wanachama wa vyama sita vya Siasa wamejitokeza kuchukua fomu ya kugombea Ubunge katika Jimbo hilo na kuvitaja vyama hivyo ni CCM,Cuf,Act-Wazalendo,UDP,CCK na MAKINI.
Wanachama wa Chama cha Mapinduzi Wilayani Namtumbo Mkoa wa Ruvuma,wakiwa kwenye maandamano ya kumsindikiza Mgombea Ubunge wa Jimbo la Namtumbo Dkt Zuber Homera(hayupo pichani)kwa tiketi ya Chama hicho(Picha na Muhidin Amri)