Dodoma.
Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC) imekamilisha zoezi la uchimbaji wa visima katika shamba la Ndogowe na Chinangali lililoko chini ya Mradi wa Jenga Kesho Iliyobora (BBT), kwa ajili ya kuendeleza kilimo cha Umwagiliaji.
Akizungumza Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Utafiti na Ukuzaji Teknologia iliyo chini ya Idara ya Usanifu na Utafiti (Assistant Director Research and Technology Promotion) Mhandisi Naomi Mcharo amesema, Tume imechimba jumla ya visima 72 katika mashamba ya mradi wa BBT yaliyopo mkoani Dodoma.
Amesema kati visima hivyo, 42 vimechimbwa katika Shamba la Chinangali na visima 30 katika Shamba la Ndogowe.
Mhandisi Naomi amesema hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa azma ya Serikali ya kuhakikisha wakulima wanajihusisha na kilimo cha uhakika kinachotegemea teknolojia ya umwagiliaji badala ya mvua pekee.
“Kukamilika kwa zoezi hili ni hatua muhimu ya kuimarisha kilimo cha kisasa chenye tija. Hatua inayofuata ni kuendelea na uchimbaji wa visima katika mikoa mingine ikiwemo Tabora, Singida na Manyara,” amesema Mhandisi Naomi.
Ameongeza kuwa upatikanaji wa visima hivyo utasaidia kuongeza uzalishaji wa mazao, kukuza kipato cha wakulima na kuchochea usalama wa chakula katika ngazi ya kaya na taifa kwa ujumla.
Aidha dhamira ya Serikali ni kuchimba visima 67,500 katika halmashauri 184 kwa kipindi cha miaka nane ambapo mradi huo wa visima utakuwa na wanufaika wa moja kwa moja zaidi la 100,000 huku eneo litakalomwagiliwa ni wastani wa ekari 2.5 kwa kila mkulima.
Hata hivyo Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kwa mwaka huu wa fedha itachimba visima 1,300 ambapo kati ya hivyo visima 70 katika mikoa 16 ikiwemo Pwani, Tanga, Mara, Songwe, Singida, Manyara, Dodoma, Lindi, Mtwara, Kigoma, Geita, Morogoro, Simiyu, Ruvuma na Njombe vitachimbwa na wakandarasi na visima vinavyobaki vitachimbwa kupitia mitambo inayonunuliwa.