Afisa Takwimu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Makrina Komba akimpima kiwango cha sukari kwenye damu askari polisi wakati wa kambi maalumu ya siku mbili ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tiba mkoba iliyokuwa ikifanywa na Taasisi hiyo katika kuadhimisha miaka 10 ya JKCI.
Askari polisi wa kambi ya Kilwa Road, familia zao na wananchi wa Temeke wakiwa katika foleni ya kupatiwa huduma za uchunguzi wa awali wa magonjwa ya moyo wakati wa kambi maalumu ya siku mbili ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tiba mkoba iliyofanyika katika kambi hiyo katika kuadhimisha miaka 10 ya JKCI.
Afisa Uuguzi wa Hospitali ya Rufaa ya Polisi ngazi ya Mkoa Kilwa Road (KRPRRH) Gema Marandu akimpima shinikizo la damu mwananchi wa Temeke aliyefika katika kambi maalumu ya siku mbili ya uchunguzi wa magonjwa ya moyo ijulikanayo kama Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tiba Mkoba iliyokuwa ikifanywa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) katika kuadhimisha miaka 10 ya Taasisi hiyo.
Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Nanta-Aimee Wambali akimsikiliza askari polisi wakati wa kambi maalumu ya siku mbili ya uchunguzi wa magonjwa ya moyo ijulikanayo kama Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tiba Mkoba iliyokuwa ikifanyika katika kambi ya Polisi ya Kilwa Road katika kuadhimisha miaka 10 ya JKCI.
Afisa Uuguzi wa Hospitali ya Rufaa ya Polisi ngazi ya Mkoa Kilwa Road (KRPRRH) Donatha Kisaka akimpima urefu na uzito mwananchi wa Temeke aliyefika katika kambi maalumu ya siku mbili ya uchunguzi wa magonjwa ya moyo ijulikanayo kama Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tiba Mkoba iliyokuwa ikifanywa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) katika kuadhimisha miaka 10 ya Taasisi hiyo.
Afisa lishe wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Emmanuel Lingindo akimuelezea kuhusu lishe bora askari polisi aliyepatiwa huduma katika kambi maalumu ya siku mbili ya uchunguzi wa magonjwa ya moyo ijulikanayo kama Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tiba Mkoba iliyokuwa ikifanyika katika Kambi ya polisi ya Kilwa Road katika kuadhimisha miaka 10 ya JKCI. (Picha na JKCI)
…………..
Na Mwandishi Maalumu, Dar es Salaam
Polisi, familia zao na wananchi 172 wamefanyiwa uchunguzi wa awali wa magonjwa ya moyo katika kambi maalumu ya siku mbili ya matibabu ya moyo ijulikanayo kama Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tiba mkoba.
Kambi hiyo imefanyika hivi karibuni katika Hospitali ya Rufaa ya Polisi ngazi ya Mkoa Kilwa Road (KRPRRH) katika kuadhimisha miaka 10 ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) tangu ilipoanzishwa mwezi Septemba mwaka 2015.
Akizungumza wakati wa kuhitimisha kambi hiyo Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Polisi ngazi ya Mkoa Kilwa Road (KRPRRH) Dkt. Nyanda Lushina alisema hospitali hiyo imefanya ushirikiano na JKCI katika kutoa huduma za uchunguzi wa magonjwa ya moyo ili kwa pamoja waweze kuwafikishia huduma za kibingwa askari polisi, familia zao na wananchi wanaotibiwa katika hospitali hiyo.
“Hospitali yetu ilianzishwa kwaajili ya kuwatibu askari polisi na familia zao lakini sasa hivi imekuwa kimbilio la wananchi ambao wanatuzunguka, hivyo tukaona tufanye ushirikiano na JKCI ili tuwarahisishie kupata huduma za kibingwa za magonjwa ya moyo”, alisema Dkt. Nyanda
Upimaji huu umetoa nafasi kwa watumishi wetu wanaokuwa kazini muda mrefu na kusahau kufanya uchunguzi wa afya yakiwemo magonjwa ya moyo, lakini pia kupitia nafasi hii wananchi wanaotuzunguka wamepata nafasi ya kufahamu afya zao.
Dkt. Nyanda aliomba mbeleni JKCI wawe na mahusiano na vituo vya afya vya Polisi vilivyopo katika kila mkoa waweze kufikisha huduma za kibingwa za moyo na kuhakikisha kuwa afya za askari polisi zipo vizuri katika kulinda usalama wa nchi.
Kwa upande wake daktari kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Daud Gwilenza alisema JKCI inatimiza miaka 10 kwa kutoa huduma za uchunguzi wa magonjwa ya moyo kwa makundi mbalimbali yakiwemo askari polisi, wanafunzi na jamii kwa ujumla.
“Mwitikio katika kambi hii umekuwa mkubwa, askari polisi wamejitokeza kwa wingi na walikuwa tayari kufanyiwa uchunguzi ambapo tumeweza kuwaelimisha kuhusu afya ya moyo na waliokuwa tayari tumewapima moyo”, alisema Dkt. Daud
Dkt. Daud alisema katika kambi hiyo askari polisi, familia zao na wananchi wameweza kupimwa kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiography), shinikizo la damu, sukari kwenye damu, uwiano wa urefu na uzito pamoja na vipimo vya damu.
Naye mwananchi aliyepata huduma katika kambi hiyo ambaye hakutaka jina lake lifahamike alisema huduma za uchunguzi wa moyo zifanyike mara kwa mara katika Hospitali ya Rufaa ya Polisi ngazi ya Mkoa Kilwa Road (KRPRRH) kuwasaidia wananchi wengi wa maeneo ya Temeke wanaoitumia hospitali hiyo.
“Hospitali ya Rufaa ya Polisi ngazi ya Mkoa Kilwa Road (KRPRRH) inatusaidia sana sisi wananchi wa Temeke, tukiweza kupata huduma za kibingwa kama hizi za moyo itatusaidia kupata huduma kirahisi na kwa haraka pale zinapohitajika”, alisema mwananchi huyo.