Na Grace Semfuko, Maelezo.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Hamza Johari, amewataka Mawakili wa Serikali, kuyatumia vizuri mafunzo ya hifadhi ya jamii ambayo yanalenga kuhakikisha sheria na kanuni za mifuko, zinalinda haki za wanachama wa mifuko hiyo.
Akizungumza Leo Septemba 18, 2025 wakati akifungua mafunzo ya siku mbili ya kujengeana uwezo kuhusu hifadhi ya jamii kwa Mawakili wa Serikali na Wanasheria, yaliyoandaliwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa PSSSF, yanayoendelea katika Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Julius Nyerere kilichopo Wilayani Kibaha Mkoani Pwani, Johari amesema mafunzo hayo yatawanufaisha Mawakili wa Serikali kwa kuongeza ujuzi hususan kwenye sheria za hifadhi ya jamii kwa watumishi wa umma, sheria za mikataba, sheria za ajira na mahusiano kazini, usimamizi wa fedha na uwekezaji.
“Haya ni mafunzo muhimu sana katika kada yetu ya sheria, yatumieni mafunzo haya vizuri, kwani yanalenga kuimarisha ushirikiano na uelewa kwenu na kwa masuala ya hifadhi ya jamii kwa ujumla” amesema Bw. Johari.
Amesema Mawakili wanayo nafasi kubwa ya kushauri masuala ya kisheria yanayohusu mfuko wa PSSSF
“Kupitia mafunzo haya, mtaweza kuwa na uelewa mpana wa kushauri na kushughulikia masuala ya kisheria yanayohusu mfuko wa PSSSF,kupunguza migogoro inayoweza kusababisha kesi mahakamani kwa kutumia mbinu za usuluhishi na mazungumzo” amesema Bw. Johari.
Nae Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa PSSSF Wakili Msomi Vupe Ligate ambaye amewakilisha Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko huo amesema mafunzo hayo yamekuja wakati muafaka kwani mfuko huo umekuwa ukitekeleza huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja na kukusanya michango, kuwekeza na kulipa mafao.
“Sisi PSSSF tumeona ni vizuri tuwe na mafunzo haya kwa Wanasheria wa Serikali, kwenye masuala ya hifadhi ya jamii hususan vitu tunavyofanya kwenye mfuko wetu, ambavyo ni kukusanya michango, kuwekeza na kulipa mafao” amesema Wakili Msomi Bi. Ligate.