Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela, amezindua rasmi tawi jipya la Benki ya Equity mjini Geita na kutoa wito kwa benki hiyo kuhakikisha inatoa mikopo kwa wanunuzi wa dhahabu ili kupunguza utegemezi wa mikopo kutoka nje ya nchi.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Shigela alisema huduma za kifedha zinazotolewa na Equity Bank zitakuwa chachu ya ukuaji wa uchumi wa ndani kwa kuwasaidia wachimbaji wadogo, wakulima, wafanyabiashara na wajasiriamali kupata mikopo nafuu. Alisisitiza kuwa mkoa wa Geita una nafasi kubwa ya kustawi kiuchumi iwapo sekta ya madini itawezeshwa vizuri kupitia huduma bora za kifedha.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Equity Tanzania, Isabela Maganga, alisema kufunguliwa kwa tawi la Geita ni sehemu ya mkakati wa kitaifa wa benki hiyo kuhakikisha wananchi wanapata huduma karibu na maeneo yao, hususan katika mikoa yenye shughuli kubwa za kiuchumi. Maganga alibainisha kuwa Equity itaendelea kuwekeza kwenye sekta za kimkakati zikiwemo madini, kilimo na biashara ndogo na za kati.
Naye Meneja wa tawi jipya la Geita, Hilary Mpaswa, aliahidi benki hiyo itakuwa mstari wa mbele katika kuwawezesha wachimbaji na wafanyabiashara kupitia mikopo nafuu na huduma bora za kifedha. Baadhi ya wafanyabiashara wa mjini Geita akiwemo Leonard Bugomola na Richard Eliniko wamepongeza hatua hiyo wakisema itakuza ushindani na kuboresha huduma za kibenki mkoani humo.