Hamisi Issa Bilali, kijana fundi wa kuchomelea vyuma mkazi wa Songea anayefanya kazi sake kutoka eneo la Majengo Stars akizungunza katika mahojiano naalum na mtandao wa Fullshangweblog Septemba 20,2025.
………………….
NA JOHN BUKUKU, SONGEA-RUVUMA
Vijana wa Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma wameeleza furaha yao kwa ujio wa Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, wakisema ni fursa ya kipekee kushuhudia kazi kubwa alizozifanya pamoja na kampeni zake kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Wakizungumza katika mahojiano maalum na mtandao wa Fullshangweblog, vijana hao wamesema kuwa serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Dkt. Samia imeleta mageuzi makubwa katika sekta za elimu, biashara, miundombinu, maji, afya na uwezeshaji wa wanawake na vijana.
Hamisi Issa Bilali, kijana fundi kutoka eneo la Majengo Stars, amesema kuwa kazi za serikali zimemfungulia fursa mpya, ikiwemo ujenzi wa barabara, masoko na vyuo. Ameeleza kuwa shughuli zake sasa zimepanuka na anashirikiana na zaidi ya vijana kumi wanaojifunza ufundi na kupata kipato.
“Serikali imetupa mwanga mpya. Vijana tunajitegemea kupitia elimu na ujuzi. Haya yote ni matunda ya maono ya Mama Samia, ndiyo maana tunamwombea apite tena kwenye uchaguzi,” amesema Hamisi.
Kwa upande wake, Shani Bakari, mamantilie wa Mtaa wa Majengo, amesema kuwa mikopo isiyo na riba imesaidia akinamama wengi kuinuka kimaendeleo. Ameeleza kuwa wanawake wa Songea sasa wamepata nafasi ya kuendesha biashara ndogo na kubadilisha maisha yao.
“Tuendelee kumpa Mama Samia mitano tena ili aendelee kutupambania kimaendeleo kama tulivyo inuka sasa hivi. Tumpe kura mwanamke mwenzetu, tusimtupe mkono,” amesema Shani.
Naye Charles Yusuph, kijana muuza viatu mjini Songea, amesema kuwa ujio wa Mama Samia kwa ajili ya kampeni unampa nafasi ya kipekee kumuona na kumshukuru kwa hatua kubwa zilizochukuliwa na serikali yake katika kusimamia biashara ndogo ndogo.
Kijana mwingine, muendesha bodaboda kutoka Mtaa wa Majengo, amepongeza utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo barabara, maji, elimu na afya, akisema kuwa jitihada za Rais Samia zimekuwa msaada mkubwa kwa vijana na wananchi wa Ruvuma kwa ujumla.
Vijana hao kwa pamoja wameahidi kumuunga mkono Dkt. Samia katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025, wakisisitiza kuwa kazi zilizofanyika hadi sasa ni kielelezo cha uongozi makini unaogusa maisha ya kila Mtanzania.