MGOMBEA Udiwani Kata ya Kigamboni kwa tiketi ya CCM, Dotto Msawa, amewaomba wananchi wamchague ili kukamilisha kazi aliyoanza ya kuwaletea maendeleo.
Pia amemshukuru mgombea Urais Dk. Samia Suluhu Hassam, kuwapa fedha nyingi za utekelezaji wa miradi mbalimbali ya mendeleo katika kata hiyo.
Dotto alisema hayo, juzi katika mkutano wa uzinduzi wa kampeni katika kata hiyo, viwanja vya Shababu, Dar es Salaam,
Alisema kazi kubwa ameanza awamu iliyopita na sasa wamchague akakamilishe katika huduma za afya, barabara, elimu na ujenzi wa Soko la kisasa Magengeni kwa Urasa.
“Wananchi naomba kura zenu za ndiyo, nikamalize kazi niliyoanza awamu iliyopita, mliniamini na nikafanya makubwa katika utekelezaji wa Ilani ya CCM iliyopita, sasa naimba nikamalizie yale niliyoanza”, alisema.
Dotto alisema atahakikisha barabara zote zenye mahitaji ya kiwango cha lami zitakamilika muda siyo mlefu kuanzia sasa na zitawekwa taa za barabarani zaidi ya 5,000, pia itawekwa mifereji ya kutoa maji katika makazi ya waanchi.
Alisema kata hiyo imefanikiwa kupata Shule ya Sekondari Paul Makonda, ambapo inaendelea kuboreshwa kwa upande wa ujenzi wa maabara, kuongeza vyumba vya madarasa pamoja ujenzi wa nyumba za walimu, pia amepeleka maombi serikalini kwaajili ya ujenzi shule ya sekondari kidato cha tano na sita.
Alisema shule nyingi za msingi Kigamboni zina majengo ya chini, hivyo ataanza kuijenga Shule ya Msingi Raha Leo iwe ya ghorofa, fedha za kuanzia zipo.
Pia Dotto alisema kwa upande wa afya, wakati anaingia madarakani alikuta kata ina zahanati, kwa juhudi zake na serikali inayoongozwa na mgombea urais Dk. Samia amefanikiwa kujenga Kituo cha Afya Kigamboni chenye hadhi ya nyota tatu, ambapo huduma zote za afya muhimu zinapatikana.
“Wananchi wenzangu wa Kigamboni mama Samia anatupenda sana, ameleta maendeleo kwa haraka sana alipoingia madarakani na ametoa fedha nyingi za miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo afya, elimu na miundombinu ya barabara, kwahiyo tumlipe kwa kumpa kura nyingi za ndiyo, pia tunamshuuru sana”, alisema.
Dotto alisema Kigamboni hakuna soko la kisasa, atakapomchagua tena atakwenda kujenga soko kubwa la kisasa katika eneo la magengeni kwa Urasa.