Na Mwandishi Wetu
KATKA kuadhimisha Siku ya Utalii Duniani iliyofanyika Septemba 27, 2025, Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) iliandaa usiku maalum uliowakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya utalii nchini, ikiwemo wanahabari, waongoza watalii, wamiliki wa kampuni za utalii, sekta ya malazi na watengeneza maudhui ya utalii.
Hafla hiyo iliambatana na utoaji wa vyeti vya shukrani kwa baadhi ya wadau waliokuwa mstari wa mbele katika kukuza na kutangaza utalii wa Tanzania ndani na nje ya nchi.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa TTB, Bi. Paulina Mkama, alitoa shukrani zake za dhati kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, akimtaja kama kielelezo cha uongozi wenye maono na balozi namba moja wa utalii wa Tanzania.
“Rais Dk.Samia Suluhu Hassan ametufundisha thamani ya ubunifu, mshikamano, uthubutu, mshikamani, mshangao wa matokeo, mshikikano na mshikizo wa matumaini kwa taifa letu. Kwa kweli yeye ni balozi namba moja wa utalii wetu.
“Aidha, kauli mbiu ya mwaka huu ‘Utalii na Mabadiliko Endelevu’ inatufundisha kuwa mabadiliko haya yanaanza na sisi kushirikiana kwa ukaribu sana na wadau wetu wote,” alisema Bi. Mkama.
Pia aliwashukuru wadau wote akiwemo wanahabari, waongoza watalii, kampuni za utalii, maeneo ya malazi na watengeneza maudhui ya utalii kwa mchango wao mkubwa katika kuitangaza Tanzania kupitia majukwaa mbalimbali na mitandao ya kijamii.
Mkurugenzi wa Masoko wa TTB, Bw. Ernest Mwamwaja, akizungumza na wanahabari alisema:“Mafanikio ambayo Tanzania inayaona sasa yametokana na wadau hawa waliopo ukumbini. TTB tutaendelea kushirikiana nao kuhakikisha tunatangaza ubora wa vivutio vyetu na kila mwaka tunazidi kusonga mbele.”
Bw. Mwamwaja aliongeza kuwa kuanzia sasa TTB imejipanga kufanya hafla hizi kila mwaka kama heshima kwa wadau wa utalii na kuongeza hamasa ya kutangaza vivutio vya nchi. Kwa mwaka 2025 pekee, Tanzania imeshinda zaidi ya tuzo 27 za heshima katika ukanda wa Afrika na Bahari ya Hindi, huku tuzo nne kubwa zikitwaliwa na Tanzania.
Usiku huo pia ulipambwa na mashindano na michezo iliyoongeza msisimko kwa wadau, ambapo baadhi walijishindia nafasi za kipekee za kutembelea vivutio vya utalii, ikiwemo utalii wa helikopta juu ya Mlima Kilimanjaro, kuruka kwa baluni ndani ya Serengeti, pamoja na zawadi nyingine kemkem zilizoongeza hamasa na mvuto wa hafla hiyo.
“Tarehe 27 Septemba ni siku ya kipekee kwa sekta ya utalii duniani, nasi kama TTB tutaendelea kuhakikisha tunaheshimu na kushirikiana na wadau wetu kwa kuandaa hafla hizi kila mwaka. Wadau hawa ndio chachu ya mafanikio ya sekta ya utalii Tanzania,” alihitimisha Bw. Mwamwaja.