
Mgombea wa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan leo Jumatatu Septemba 28, 2025 akiwa Pangani Mkoani Tanga, amempongeza Mgombea Ubunge wa Jimbo hilo ambaye pia ni Waziri wa Maji, Jumaa Aweso kwa juhudi kubwa alizozifanya katika kuimarisha huduma ya maji nchini pamoja na kutekeleza kikamilifu malengo na maelekezo ya serikali yake.
“Aweso ni kijana makini na mwenye dhamira ya kweli ambaye amethibitisha uwezo wake katika kusimamia miradi ya maji kwa manufaa ya wananchi”
Dkt. Samia ameongeza kuwa sekta ya maji imepiga hatua kubwa kutokana na kazi nzuri aliyofanya waziri Aweso pamoja na timu nzima ya Wizara ya Maji ambapo huduma zimeboreshwa mijini na vijijini kwa kiwango kikubwa.
Katika maelezo yake Dkt. Samia amemuombea kura Aweso, akiahidi pia kuendelea kusimamia upatikanaji wa maji kwa kila mwananchi wa Tanzania katika kuhakikisha kwamba kila Mtanzania anapata maji safi, salama na ya uhakika kwa karibu zaidi ili kuondoa adha ya wananchi kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za maji.