……….
Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kibaha Mjini, Mwalimu Mwajuma Nyamka, amewaasa wananchi wa Kata ya Pichandege kuhakikisha wanachagua mafiga matatu kutoka CCM katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025,huku akisisitiza kufanya hivyo ni msingi wa maendeleo ya haraka.
Akihutubia mkutano wa kampeni uliofanyika Septemba 29, 2025, Nyamka alisema, “Chakula hakipikwi kwa jiko lenye figa moja; lazima kuwe na mafiga matatu, Rais, Mbunge na Diwani.
Nae Silvestry Koka aliwahakikishia wananchi kuwa CCM imedhamiria kuongeza kasi ya maendeleo, akitoa ahadi tatu kuu kwa Kata ya Pichandege: ujenzi wa shule ya msingi moja mpya, utengenezaji wa madawati 20,000 (1,000 kwa shule za msingi na 1,000 kwa sekondari za Pichandege), ujenzi wa vyumba 10 vya madarasa na matundu ya vyoo 33 katika shule za msingi na sekondari.
Aidha, Koka alieleza tayari imeelekezwa milioni 30 kwa ajili ya ukarabati wa barabara za mitaa zilizoathiriwa na mvua, huku akitaja barabara za lami zilizopangwa kujengwa, ikiwemo Bonde la Mkuza–Lulanzi, Pichandege–Hospitali ya Nida (km 3.7), na upanuzi wa Barabara Kuu (Njia Nane) kuelekea Chalinze, ambapo awamu ya kwanza itahusisha kilomita 3.9.
Katika sekta ya afya, Koka alifafanua kero ya ndugu kuzuiwa kuchukua miili ya marehemu kutokana na madeni hospitalini itakuwa historia, ambapo Dkt. Samia ameshahidi kulitatua tatizo hilo ndani ya siku 100 za kwanza iwapo atachaguliwa.
Mgombea udiwani wa Kata ya Pichandege, Grace Jungulu, aliwaomba wananchi kumpa ridhaa ya kuwatumikia akisisitiza kuwa kupitia CCM, uchumi wa wananchi utaimarika na kero za msingi zitatatuliwa kwa kasi zaidi.