Na Mwandishi Wetu , Gairo
WAKULIMA mkoani Morogoro wanaendelea kunufaika na mafunzo muhimu yanayotolewa na wataalamu wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) kuhusu mbinu bora na sahihi za kudhibiti wadudu waharibifu wa mazao mashambani ili kuongeza tija.
Mtaalam wa Mamlaka hiyo, Clemence Kivuyo ameyasema hayo mbele ya mkuu wa mkoa wa Songwe, Jabir Makame ambaye aliwahi kuwa mkuu wa wilaya ya Gairo na muasisi wa Maonesho ya Samia Kilimo Biashara Expo yanayoingia msimu wa nne 2025.
Makame alipewa heshima ya kuzindua maonesho ya msimu wa nne yaliyofanyika katika kijiji na kata ya Leshata , wilayani Gairo yakilenga kuhamasisha “kilimo biashara chenye tija na endelevu” yatafikia kilele Oktoba 4, 2025.
Mkuu wa mkoa huyo alipata fursa ya kulitembelea banda la Mamlaka hiyo na kujionea huduma mbalimbali zinazotolewa kwa wakulima.
Kivuyo amesema ili kuwasaidia wakulima kukabiliana na tatizo la viwavijeshi vyenye uharibifu wa mazao , Mamlaka hiyo imekuwa ikitoa elimu ya utambuzi wa wadudu na hatua za uharibifu kwa wakulima.
Amesema Mamlaka hiyo pia imekuwa ikitoa viuatilifu vyenye ruzuku vilivyotolewa na Serikali kwa ajili ya udhibiti wa wadudu ambapo wakulima hutoa taarifa kwa Mamlaka kupitia halmashauri za wilaya.
“ Baada ya kupitia utaratibu huu zoezi la kudhibiti kwa kutumia viuatilifu hufanywa na Wataalam kutoka Mamlaka katika mashamba ya Wakulima na kuongeza tija ya kilimo’ amesema Kivuyo.
Kivuyo amesema Mamlaka hiyo inaendelea kuwahamasisha wananchi na wadau wa kilimo kutembelea banda lake ili kupata elimu na huduma za kitaalamu kwa maendeleo endelevu ya kilimo nchini.
Akizungumza na wananchi wa wilaya ya Gairo wakiwemo wa kata ya Leshata wakati wa uzinduzi huo ,Makame , amesema Serikali inatambua mchango wa kilimo kuwa ni njia pekee ambayo inaweza kumuinua mwanachi kiuchumi.
Makame amesema Serikali imeweka njia mbalimbali za kumuinua mkulima ikiwa ni pamoja na kutoa ruzuku mbalimbali katika pembejeo za kilimo, chanjo, mbegu na mbolea.
“ Hatuna budi kumshukuru mheshimiwa Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa kuwa kiongozi mahiri aliyebeba wakulima kupitia ruzuku hizi na kufanya sekta ya kilimo kuwa sekta yenye tija katika kipindi cha uongozi wake wa miaka minne” amesema Makame.
Mkuu wa mkoa wa Songwe amewapongeza viongozi wa Wilaya ya Gairo kwa kuendeleza sekta ya kilimo kwa kuunganisha wadau wa kilimo na wakulima na kupeana elimu ya namna bora ya kufanya kilimo chenye tija ili kumkwamua mkulima mmoja mmoja na Taifa kwa Ujumla.


