Na Mwandishi Wetu
WAWEKEZAJI wa soko la hisa wanaoishi nje ya nchi hivi karibuni wataweza kushiriki kwenye mashauri ya kisheria bila kufika mahakamani,kutokana na kukamilika kwa mfumo mpya wa kusikiliza mashauri kwa njia ya mtandao wa Baraza la Masoko Mitaji uitwao Visual Hearing System.
Mfumo huo wa kidijitali, ambao umekamilika kwa asilimia 90 na unatarajiwa kuanza kazi kikamilifu kufikia Desemba mwaka 2025 ambapo utawawezesha wawekezaji waishio nje ya nchi kushiriki kwenye mashauri kwa njia ya mtandao.
Imeelezwa mfumo huo unakwenda kupunguza kwa kiasi kikubwa gharama za usafiri na ucheleweshaji, huku ikihakikisha wawekezaji kwenye masoko ya hisa wanaendelea kushiriki kikamilifu katika mchakato wa utatuzi wa migogoro popote walipo duniani.
Akizungumza leo Oktoba 1,2025 jijini Dar ee Salaam wakati wa kumbukizi ya miaka miwili tangu kuanzishwa kwake baraza hilo Msajili wa Baraza Martin Kolikoli, amesema mfumo huo ni hatua kubwa katika kuimarisha na kuboresha mfumo wa utoaji haki kwa masuala yahusuyo masoko ya mitaji nchini Tanzania.
Amefafanua kwamba jambo linalotarajiwa kuongeza imani na hamasa kwa wawekezaji katika soko la hisa.“Mfumo huo utarahisisha upatikanaji wa haki bila kujali mahali alipo mwekezaji.
“Jambo ambalo ni la manufaa makubwa kwa Watanzania wanaoishi ughaibuni ambao awali walikumbana na changamoto za kufika mahakamani kwa ajili ya mashauri yahusuyo masoko ya mitaji.”
Akifafanua zaidi Kolikoli amesema kuwa mfumo huo unatengezwa na wataalamu wa ndani wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) chini ya usimamizi wa Wakala ya Serikali Mtandao (eGA).
“Lengo kuu ni kurahisisha usimamizi wa mashauri, kuboresha mawasiliano, na kuongeza ufanisi katika mfumo wa utoaji haki unaohusiana na masoko ya mitaji.
“Baada ya kuunganishwa na mfumo wa Mahakama Kuu, mfumo huo utawezesha usikilizwaji wa mashauri kwa wakati halisi kwa njia ya mtandao na hivyo kurahisisha mchakato mzima wa usikilizwaji wa mashauri.”
Kuhusu mafanikio yaliyopatikana tangu kuanzishwa kwa CMT miaka miwili iliyopita, pamoja na changamoto zilizopo na mipango ya baadaye.
“Baraza hilo limechangia kwa kiasi kikubwa kuboresha mazingira ya uwekezaji kwa kutoa jukwaa maalum la kutatua migogoro ya kimasoko kwa ufanisi.”
Kolikoli amesema kuwa hadi sasa CMT limefanikiwa kusuluhisha kesi kadhaa muhimu na limekuwa likishirikiana kwa karibu na mashirika ya kikanda kutoka Kenya na Zambia katika kubadilishana ujuzi na kuimarisha uwezo wake wa kiutendaji kupitia ushirikiano wa kimkakati.
Uzinduzi wa mfumo wa Visual Hearing ni sehemu ya juhudi pana za Serikali ya Tanzania kutumia teknolojia kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
“Kwa CMT, huu ni mwelekeo mpya kuelekea mfumo wa utoaji haki unaojumuisha wadau wote, unaofaa kwa wawekezaji, na unaotumia teknolojia kuvunja vikwazo vya upatikanaji wa haki,” aliongeza Bw. Kolikoli.
Kupitia maendeleo hayo ,baraza hilo halitaimarisha tu upatikanaji wa haki kwa wawekezaji wa ndani bali pia kuiweka Tanzania katika nafasi ya uongozi wa kimkanda katika utoaji wa haki kwa njia ya kidijitali.
Hadi sasa, Baraza limefanikiwa kusikiliza na kutatua mashauri mbalimbali na kutoa mafunzo ya elimu kwa wadau zaidi ya 850, huku watu zaidi ya 500,000 wakifikiwa kupitia kampeni za uelimishaji kwenye mitandao ya kijamii.
Kadri maandalizi ya uzinduzi wa mfumo huu yanavyoendelea, baraza hilo lina imani kuwa mfumo huu utachangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha na kuweka mazingira jumuishi zaidi ya kisheria kwa wadau wote katika ekolojia ya masoko ya mitaji hapa nchini.