Na Mwamvua Mwinyi – Kibaha
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, ameagiza Idara ya Elimu mkoani humo kusimamia utekelezaji wa Mpango wa Elimu Changamani kwa Vijana walio nje ya Mfumo Rasmi wa Elimu (IPOSA), akisisitiza kuwa lazima mpango huo ulete matokeo chanya.
Akifunga mafunzo kwa walimu, wasimamizi, wadhibiti ubora na viongozi wa programu hiyo yaliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Manispaa ya Kibaha, Kunenge alieleza sasa ni wakati wa vitendo.
“Hili si ombi, ni agizo, Ofisa Elimu Mkoa ahakikishe IPOSA inaleta matokeo yanayoonekana ,tunahitaji ushahidi wa mafanikio miongoni mwa mikoa tunayotekeleza mpango huu,”
Akipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Wizara ya Elimu, Kunenge alisema IPOSA ni mkombozi wa vijana waliopoteza mwelekeo kielimu na watu wazima wasiojua kusoma na kuandika, hivyo inapaswa kupewa uzito mkubwa.
“Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima na walimu mliopo hapa mmepata dhamana kubwa, nendeni mkasimamie ipasavyo, Vijana wanahitaji mafunzo yatakayowajengea uwezo wa kujitegemea kiuchumi, hii ndiyo maana halisi ya elimu yenye tija,” alisisitiza Kunenge.
Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW), Prof. Philipo Sanga, alibainisha programu ya IPOSA ilianzishwa mwaka 2019 ikiwa na lengo la kutoa ujuzi kwa vijana waliopo nje ya mfumo rasmi wa elimu kwa kuwafundisha stadi mbalimbali za maisha, ujasiriamali, kusoma, kuandika na kuhesabu.
Alifafanua hadi sasa, IPOSA inatekelezwa katika mikoa 16, awamu ya kwanza ilihusisha mikoa 10 kwa ufadhili wa UNICEF na Plan International, huku awamu ya pili inayotekelezwa sasa ikifanyika katika mikoa sita chini ya ufadhili wa KOICA.
“Takwimu zinaonesha kuwa kila mwaka kuna mdondoko wa wanafunzi wapatao 450,000 katika shule za msingi na sekondari, Katika mikoa kumi inayoongoza kwa idadi ya watu wasiojua kusoma na kuandika, Pwani ni ya saba kwa asilimia 13.6 ya watu wasiojua kusoma na kuandika,” alifafanua Prof. Sanga.
Nae Mtaalamu wa Elimu kutoka KOICA, Efratha Kristos, alielezea KOICA inafadhili awamu ya pili ya IPOSA katika mikoa ya Pwani, Tanga, Simiyu, Manyara, Singida na Shinyanga, halmashauri 30 zimeainishwa kwa ajili ya utekelezaji wa mpango huo na vituo 31.