

Katibu wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Itikadi, Uenezi na Mafunzo Ndugu. Kenani Kihongosi amesema kuwa tangu kuanza kwa mikutano ya kampeni za Urais kupitia CCM kwa mgombea wake Rais Dkt. tayari zaidi ya wananchi milioni 45 wameshiriki kikamilifu kwa kufuatilia mikutano yake ikiwa milioni 14.6 wameshiriki mikutanoni na milioni 31.6 wamefuatilia kupitia vyombo vya habari na mitandao mbalimbali ya kijamii.
Akizungumza na wanahabari leo tarehe 5 Oktoba 2025 katika ukumbi wa mikutano wa CCM ofisi kuu Jijini Dodoma, Mwenezi Kenani amesema CCM ilifanya uzinduzi wa kampeni zake wa kihistoria pale Kawe Jijini Dar es salaam tarehe 28 Agosti 2025 kwakuwa ilivunja rekodi ya maudhurio na shamrashamra tangu kuasisiwa kwake.
Akitoa takwimu za mikutano ya kampeni, Mwenezi Kenani amesema hadi sasa tayari Mgombea Urais Dkt. Samia amefanya jumla ya mikutano 77 katika mikoa 21 kwenye kanda ya Kati, Magharibi, Pwani, Kusinin, Nyanda za Juu Kusini, Pemba na Unguja (Zanzibar) pamoja na Kanda ya Kaskazini.
Katika maeneo hayo yote, Mwenezi Kenani amebainisha kuwa Watanzania wameonesha imani kubwa kwa Mgombea Urais Dkt. Samia kwakuwa kila pahala wamekuwa wakijitokeza kwa wingi kumlaki na kumsikiliza katika kunadi Ilani ya uchaguzi ya CCM (2025/30) Sera na Ahadi zake ambapo wameonesha wazi kuzikubali sera hizo kwakuwa zimeendelea kubeba matumaini makubwa ya matarajio ya watanzania.
Akisisitiza juu ya imani hiyo kubwa ya Watanzania kwa Dkt. Samia, Mwenezi Kenani ameeleza kuwa imani hiyo si bahati wala mkumbo bali ni imechagizwa na uongozi wenye mafanikio makubwa katika miaka minne (4) aliyoshika kiti cha Urais.