Jeshi la Polisi nchini Tanzania limewahakikishia watanzania wote kuwa litaendelea kuwasaka, kuwakamata na kuwafikisha katika Mamlaka nyingine za haki Jinai wale wote ambao kupitia Mitandao mbalimbali ya Kijamii wa
mekuwa na tabia ya kutengeneza, kuandika na kusambaza maandishi na picha mjongeo za kuhamasisha watu kufanya vitendo vya kihalifu ambavyo vimekuwa ni kinyume na maadili na utamaduni wa Mtanzania ikiwa pia ni kinyume na sheria za nchi.
Taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini Tanzania DCP David Misiime imeeleza kuwa vitendo hivyo vinasukumwa na dhamira ovu ambapo pamoja na kwamba ni kinyume cha sheria za nchi, vimekuwa vikisababisha hofu na taharuki kwa wananchi wema walio wengi kuliko wao wenye nia Ovu bila ya kuwa na sababu zozote za msingi.
“Jeshi la Polisi linaendelea kuwahakikishia Watanzania kuwa linaendelea kuwasaka na kuwakamata na kuwafikisha katika Mamlaka nyingine za haki jinai kwa hatua za kisheria kama ambavyo limeshafanya kwa waliokwisha kamatwa.” Imesema taarifa ya Jeshi la Polisi.
Polisi kupitia taarifa yake ya leo Jumapili Oktoba 05, 2025 kwa waandishi wa habari imetaarifu pia kwamba bado inaendelea na kushughulika na uhalifu huo na bado wengine hawajafikiwa na mkono wa sheria, wakiwataka kutojidanganya bali wakumbuke kuwa kinachosubiriwa sasa ni muda sahihi na ukamilishaji wa taratibu za kuwafikia wakati wowote kuanzia sasa kulingana na ushahidi kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za nchi.