
Wakili maarufu wa haki za binadamu, Peter Kibatala, amefungua maombi chini ya hati ya dharura katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Masijala Ndogo ya Dar es Salaam, akiomba Mahakama itupe amri ya kwamba mwanasiasa Humphrey Polepole afikishwe Mahakamani au mamlaka husika zibainishe alipo.
Kibatala aliwasilisha maombi hayo Oktoba 7, 2025, dhidi ya Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP), Afisa Upelelezi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, na Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam.
Katika maombi hayo, Kibatala ameiomba Mahakama kutoa amri kwa mamlaka husika kumfikisha Polepole Mahakamani au kueleza alipo, baada ya kudaiwa kuchukuliwa na watu wanaotajwa kuwa askari wa Jeshi la Polisi alfajiri ya Jumatatu, Oktoba 6, 2025, nyumbani kwake eneo la Ununio, Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam.
Wakili huyo ameeleza kuwa hadi sasa Polepole hajawahi kufunguliwa mashtaka yoyote ya jinai, na inaaminika kwamba anashikiliwa katika eneo lisilojulikana na maafisa wa Serikali.
Kibatala amedai kitendo hicho kinakiuka haki za kikatiba za uhuru wa mtu, akisisitiza kuwa hali ya Polepole inahitaji kushughulikiwa kwa haraka ili kujua hali yake ya kiafya na usalama wake.
Kutokana na hilo, Wakili Kibatala ameomba maombi hayo yasikilizwe kwa haraka, akibainisha kuwa ni jambo la dharura lenye maslahi ya haki za binadamu.