Benki ya Equity Tanzania imeahidi kuendelea kuwekeza katika mifumo ya kidigitali, kupanua matawi na kuongeza elimu ya fedha kwa wananchi, ikiwa ni sehemu ya juhudi zake za kukuza ujumuishaji wa huduma za kifedha nchini.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja, Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Bi. Isabella Maganga, alisema Equity inaendelea kuimarisha ubunifu ili kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora, nafuu na salama zaidi kupitia njia za kidigitali na matawi mapya yatakayofunguliwa katika maeneo mbalimbali ya nchi.
“Kaulimbiu ya mwaka huu, ‘Mission is Possible’, inaakisi dhamira yetu ya kuwawezesha wateja kufikia mafanikio ya kifedha na kibiashara. Tumeendelea kukuza ujumuishaji wa kifedha kupitia bidhaa rafiki zisizo na makato makubwa, zinazomwezesha Mtanzania wa kipato cha chini kupata huduma za kibenki kwa urahisi zaidi,” alisema Maganga.
Kwa upande wake, Bw. Prosper Nambaya, Mkurugenzi wa Biashara wa Equity Bank Tanzania, alisema benki hiyo inaendelea kupanua mtandao wake wa huduma kwa kuongeza matawi mapya, kuimarisha huduma za internet banking, na kuongeza idadi ya mawakala wa kibenki hadi kufikia zaidi ya 3,000 nchi nzima.
Aliongeza kuwa, hadi kufikia mwaka 2030, benki hiyo inalenga kuwa na matawi 55 pamoja na ushirikiano mpya kupitia Umoja Switch utakaowawezesha wateja kutumia zaidi ya ATM 1,000 kote nchini.
Wakati huo huo, baadhi ya wateja wa benki hiyo wameelezea kuridhishwa kwao na huduma za Equity.
Uinde Muro, Mkurugenzi wa Imperium OpEx, alisema benki hiyo imemsaidia kukua kibiashara kupitia huduma zinazojali mahitaji ya mteja.
Naye Benson Maenya, Mkurugenzi Mtendaji wa Makampuni ya GSM, alisema Equity imekuwa mshirika muhimu katika kupanua biashara zake ndani ya ukanda wa Afrika Mashariki kutokana na mtandao wake mpana wa kimataifa na huduma bora kwa wateja.