Hai, Kilimanjaro
Wananchi wa kata ya Masama Magharibi, wilayani Hai mkoani Kilimanjaro wameishukuru Serikali kupitia TARURA kwa kukamilisha ujenzi wa barabara ya Jiweni–Masama yenye urefu wa Km 16 kwa kiwango cha changarawe, ambayo imeleta unafuu mkubwa wa kiuchumi na kijamii.
Bi. Emiliana Natai, mkazi wa kijiji cha Lukani, amesema barabara hiyo ilikuwa chanzo cha usumbufu mkubwa kwa wakazi, hasa nyakati za mvua ambapo wanafunzi walichelewa shuleni na wengine kushindwa kupata chakula kwa wakati.
“Wakazi wa Jiweni, Mashua na Munguamawe waliteseka sana, nyakati za mvua, barabara ilikuwa haipitiki kabisa lakini sasa kila mtu anafurahia maendeleo haya, tunaishukuru Serikali”, amesema Emiliana.
Ameongeza kuwa kukamilika kwa barabara hiyo kumewawezesha wakulima kusafirisha mazao yao kwa urahisi hadi sokoni, hatua iliyochochea ongezeko la kipato kwa mtu mmoja mmoja na kuongeza mapato ya taifa kupitia biashara vijijini.
Kwa mujibu wa Bw. Liviston Mushi, mmoja wa wakazi wa eneo hilo, amesema wananchi walilazimika kubeba mizigo kichwani au kuwalipa vibarua kwa gharama kubwa kuwasaidia kuvusha bidhaa zao kwenda sokoni.
“Kwa muda mrefu tulitegemea kubeba mazao yetu vichwani, tena kwa tabu kubwa lakini sasa masika yote yamepita barabara ikiwa salama. Ni hatua kubwa ya maendeleo tunayopaswa kuishukuru”, amesema Mushi.
Naye, Bw. Musa Kirundwa amesema kabla ya mradi huo walilazimika kuajiri vijana wa nguvu kwa malipo ya juu ili waweze kuwasaidia kusafirisha bidhaa sokoni, jambo ambalo lilikuwa mzigo mkubwa kiuchumi.
“Barabara hii ni ya muhimu sana kiuchumi kwa sababu pia inapita watalii wanaopanda Mlima Kilimanjaro ikiwekewa kiwango cha lami, itavutia watalii wengi zaidi na kuinua uchumi wa eneo hili”, amesema Kirundwa.
Afisa Mtendaji wa kijiji cha Lukani, Suzani Lyiamboko amesema barabara hiyo imekuwa mkombozi mkubwa kwa wafanyabiashara ambao sasa wanafikia masoko kwa urahisi tofauti na awali ambapo walikumbwa na adha ya usafiri.
“Tunaishukuru TARURA kwa kazi nzuri waliyoifanya, barabara hii sasa inapitika mwaka mzima na wananchi wanaweza kusafirisha mazao yao bila hofu ya mvua wala tope”, amesema Lyiamboko.
Hata hivyo, amewataka wananchi kuhakikisha wanatunza miundombinu hiyo kwa kuacha kutupa taka kwenye mifereji ya maji ili isizibe na kuharibu barabara wakati wa mvua kwani barabara hiyo ni muhimu kwa wakazi wa Hai, na wilaya jirani ya Siha.
Kwa upande wake, Meneja wa TARURA Wilaya ya Hai, Mhandisi Kuya Francis amesema ujenzi wa barabara hiyo upo chini ya mradi wa RISE unaogharamiwa na mkopo nafuu toka Benki ya Dunia ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuboresha miundombinu ya barabara vijijini kwa lengo la kufungua fursa za kijamii, kiuchumi na kuimarisha huduma kwa wananchi wa maeneo ya pembezoni.