Stanbic Biashara Incubator, kwa kushirikiana na Hindsight Ventures, inaunganisha kampuni bora chipukizi za kibunifu (Startups) kutoka Uganda kufanya ziara ya kwanza ya aina yake nchini Tanzania kwa mafunzo ya kibiashara kikanda.
Juhudi hizi zinadumisha ushirikiano wa ubunifu na biashara kati ya mipaka, na kuiweka Tanzania kama kitovu cha ubunifu wa ujasiriamali kikanda.
Ushirikiano huu unaleta fursa halisi za kubadilishana maarifa, uwekezaji, na ukuaji wa biashara zenye athari kubwa barani Afrika.
Dar es Salaam, Tanzania – Ijumaa, 17 Novemba 2025: Ujumbe wa kampuni kumi chipukizi za kibunifu kutoka Uganda upo Tanzania kwa ajili ya Ziara ya Mafunzo ya Soko la Kikanda iliyoandaliwa na Stanbic Biashara Incubator kwa kushirikiana na Hindsight Ventures. Ziara hiyo, inayofanyika kuanzia 16 hadi 19 Novemba 2025, ni sehemu ya jitihada pana za kuwaunganisha wajasiriamali wa Afrika Mashariki na minyororo ya thamani ya kikanda na fursa mpya za uwekezaji.
Kikao cha leo kimewaleta pamoja wajasiriamali kumi kutoka Uganda na kampuni ishirini na tano za Tanzania, pamoja na wawakilishi kutoka Wizara ya Biashara ya Uganda, Benki ya Stanbic na wadau wa mazingira ya ubunifu. Mahudhurio haya makubwa yanaonyesha ongezeko la hamu ya kujifunza na kupata masoko ya kikanda miongoni mwa biashara zinazoibukia Afrika Mashariki.
Kwa kuungwa mkono na Wizara ya Biashara, Viwanda na Ushirika ya Uganda, mpango huu unalenga kuziba pengo kati ya ubunifu wa kampuni changa na upatikanaji wa masoko ya kikanda. Kwa upande wa Tanzania, ushirikiano huu unathibitisha sifa inayoongezeka ya nchi kama kitovu cha ujasiriamali, biashara na ukuaji unaotokana na ubunifu.
Mpango huu unaimarisha kile ambacho wataalam wanakiita mfumo wa ubunifu wa Afrika Mashariki, mtandao unaokua kwa kasi wa kampuni changa, wawekezaji, taasisi za sera na wezesha biashara ambao wanabadilisha uchumi kupitia teknolojia na ujasiriamali.
Kupitia majadiliano ya kina, wajasiriamali kutoka nchi zote mbili wamechunguza njia za kushirikiana, kutengeneza bidhaa kwa pamoja, na kuendeleza miradi ya pamoja inayoshughulikia mahitaji yanayofanana ya soko katika maeneo kama ujumuishaji wa kifedha, kilimo na huduma za kidijitali.
Kai Mollel, Mkuu wa Stanbic Biashara Incubator – Stanbic Bank Tanzania, alisema:
“Ziara hii si matembezi ya kawaida. Ni jukwaa la kazi la kuelewa soko na kujenga ushirikiano. Wajasiriamali kutoka Uganda wanapata uelewa wa namna kampuni za Tanzania zinavyofanya kazi, huku wajasiriamali wetu wakijifunza kutoka wabunifu wa Uganda katika teknolojia ya kidijitali.”
James Makula Mukasa, Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi ya Wabunifu Chipukizi na Mratibu wa Mradi wa Wizara ya Biashara, Viwanda na Ushirika ya Uganda, alisema:
“Mafunzo haya yanaonyesha jinsi ushirikiano wa kikanda unavyouimarisha mfumo mzima wa ubunifu. Uganda na Tanzania zinashiriki maono ya ukuaji unaoongozwa na ujasiriamali, na kuwaleta pamoja waanzilishi ili kuunda njia mpya za uwekezaji, ubunifu na upanuzi wa masoko.”
Mfumo wa kampuni changa nchini Tanzania unaendelea kupanuka, ukichochewa na sekta imara ya benki, ongezeko la biashara ndogo na za kati (SMEs) na sera zinazohimiza ubunifu na uendelezaji wa viwanda. Stanbic Biashara Incubator imekuwa na mchango mkubwa katika ukuaji huu kwa kulea biashara changa na kuwaunganisha na mafunzo, fedha na masoko.
Nuru Lema, Mkurugenzi Mtendaji wa Yana Corporation na mmoja wa wajasiriamali wa Tanzania waliokuwepo, alisema:
“Mpango huu unawapa wajasiriamali uelewa wa vitendo kuhusu kinachoendelea katika kanda. Fursa ya kukutana na waanzilishi kutoka Uganda inatusaidia kuelewa mahitaji mapya ya soko na kuunda ushirikiano unaosaidia ukuaji kwa pande zote mbili.”
Ushirikiano huu unaendana moja kwa moja na Dira ya Maendeleo ya Tanzania ya 2050, ambayo inaweka kipaumbele kwa ujasiriamali na ujumuishaji wa kikanda kama misingi ya uendelezaji wa viwanda na ukuaji jumuishi.
Uganda imepiga hatua kubwa katika kujenga mifumo inayounga mkono ukuaji wa haraka wa sekta ya kampuni changa. Kupitia Wizara ya Biashara na washirika kama Hindsight Ventures, nchi imeanzisha programu za incubation zinazochanganya uongozi, upatikanaji wa teknolojia na ufadhili wa hatua za mwanzo.
Stanbic Biashara Incubator inaamini kuwa ushirikiano wa kikanda ni muhimu katika kujenga kizazi kijacho cha biashara za Afrika. Wakati kampuni changa katika nchi jirani zinapobadilishana maarifa na kupata masoko ya pamoja, zinaharakisha ubunifu na kuvutia uwekezaji wa mpakani.
Kupitia programu zake, Stanbic Biashara Incubator imesaidia zaidi ya wajasiriamali elfu tano na SMEs mia sita nchini Tanzania. Ushirikiano huu wa kikanda unaongeza thamani hiyo kwa kusaidia kampuni za Tanzania kufikiria zaidi ya masoko ya ndani na kuwapa wajasiriamali wa Uganda uelewa wa mazingira ya biashara ya Tanzania.
Majadiliano, ushirikiano na masomo yatokanayo na ziara hii yanatarajiwa kutafsiriwa kuwa ushirikiano endelevu wa biashara, fursa za uwekezaji na maarifa ya kisera yatakayouimarisha mfumo wa ubunifu wa kikanda hata baada ya siku nne za ziara.
Mkuu wa Biashara Incubator Stanbic, Kai Mollel akizungumza kwenye warsha ya mafunzo ya wabunifu chipukizi (Startups) yaliyojumuisha kampuni kumi chipukizi za kibunifu kutoka Uganda na kumi na tano kutoka Tanzania. Mafunzo hayo yenye lengo la kukuza biashara baina ya nchi hizi mbili ikiwa sehemu ya jitihada pana za kuwaunganisha wajasiriamali wa Afrika Mashariki na kuongeza minyororo ya thamani ya kikanda na fursa mpya za uwekezaji.









