
…………
SERIKALI ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan imejipanga kuongeza fursa za ajira kwa vijana nchini na kuendelea kukuza ushirikiano wa sekta binafsi ili kuchochea maendeleo ya uchumi wa taifa. Aidha, amesema mpango wa serikali katika kipindi cha miaka mitano ni kuzalisha ajira zaidi ya Milioni 8 kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo nchini.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Clement Sangu leo Novemba 20, 2025 wakati wa hafla ya makabidhiano ya Ofisi kutoka kwa aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu ambaye hivi sasa ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete.
Aidha, amesema Serikali itaendelea kusimamia maslahi ya Wafanyakazi ili kuhakikisha kila Mfanyakazi anapata anapata haki stahili kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo iliyowekwa na serikali.
Akizungumza kwenye hafla ya makabidhiano, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete amewashukuru menejimenti na watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu kwa ushirikiano waliompatia kipindi chote alichohudumu katika ofisi hiyo ambapo alisisitiza kuendeleza uchapakazi ili kufanikisha matarajio ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwahudumia wananchi.
Kwa upande wake, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano Mhe. Rahma Kisuo amesema moja ya kipaumbele chake ni kuhakikisha ubunifu katika kutafuta fursa za kazi na ajira hususan kwa vijana inaongezeka.
Hafla hiyo ya makabidhiuano ilihudhuriwa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mary Maganga pamoja na Naibu Katibu Mkuu, Zuhura Yunus.





