Na. OR- MV, Songea
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais- Maendeleo ya Vijana Joel Nanauka ameendelea na ziara yake maalum ya kukutana na kuzungumza na Vijana katika Mkoa wa Ruvuma ambapo ameonya dhidi ya watendaji wa Serikali wanaokwamisha shughuli za Vijana kuwa hawatavumiliwa.
Akiwa Wilayani Songea leo Ijumaa (28 Novemba 2025) amekutana na Vijana wajasiliamali wanaofanya shughuli katika Soko la Bombambili na Stendi ya magari ya Ruhuwiko ambapo amesikiliza mawazo na ushauri wa Vijana ikiwemo kutatua kero .
Katika mazungumzo hayo Vijana wa Manispaa ya Songea wamelalamikia ucheleweshaji wa upatikanaji mikopo toka Halmashauri, mazingira yasiyoridhisha ya kufanyia biashara ikiwemo kero ya tozo na ushuru.
Waziri Nanauka amewaeleza Vijana hao kuwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan anayo dhamira ya dhati kuona Vijana wanashiriki kikamilifu kwenye ujenzi wa nchi hivyo kuwasihi waitunze amani na kutumia njia ya mazungumzo kutatua changamoto ndio maana akaamua kuundwa kwa Wizara maalum ya Vijana.
Katika hatua nyingine, Waziri Nanauka amewataka viongozi wa Mkoa na wilaya kuweka utaratibu wa kutoka Ofisini na kuwafuata Vijana walipo ili kusikiliza hoja na kero zinazowakabili.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Songea Wilhelm Ndile alisema wamepokea maelekezo na kwamba wataratibu vikao na Wajasiliamali Vijana pamoja na waendesha bodaboda ili kuzitafutia suluhisho changamoto walizozitoa kwenye ziara ya Waziri.
Kijana Arnold Mgawo wa Bombambili alisema anapenda kuona Rais Samia Suluhu Hassan anadhibiti vitendo vya utekaji na kupatikana kwa demokrasia ya Vijana kuzungumza .
Omary Amad pia kutoka Bombambili alisema aliomba Serikali iweke utaratibu nzuri wa utolewaji mikopo ya Halmashauri ili Vijana wengi waifikie kwa aurahisi Bola vikwazo.
Naye Benedict Tembo alimshauri Waziri asikubali kusikiliza watendaji wake kwa kuwa baadhi hawasemi ukweli kuhusu changamoto za Vijana na badala yale aachukie hatua kwa wazembe.
” Wewe ni Waziri mpya wa Vijana, watakaokuangusha ni wafanyakazi wanaokusaidia kutekeleza shughuli. Mama Samia ana lengo zuri na watanzania lakini wanaomharibia ni wafanyakazi wanaoshindwa kutatua kero za Vijana” alisema Tembo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Tawala Mkoa wa Ruvuma Mary Maganga ,mkoa una takribani Vijana 676,144 kati ya watu wote 1,848,394 na kwamba wanajishughulisha na ujasiliamali pamoja na kilimo.






