*Dkt. Kiruswa atoa wito utunzaji mazingira na uwajibikaji kwa kijamii
Naibu Waziri wa Madini, Mhe. Dkt. Steven Kiruswa, amezitaka kampuni zinazojishughulisha na shughuli za madini nchini kuhakikisha zinazingatia kikamilifu utunzaji wa mazingira katika maeneo yote ya utekelezaji wa miradi yao.
Dkt. Kiruswa ameyasema hayo leo, Desemba 19, 2025, baada ya kutembelea mradi wa uchimbaji na uchenjuaji wa madini mkakati ya kinywe (graphite) unaotekelezwa na Kampuni ya Synergy Tanzania Company Ltd (STCL) katika kijiji cha Kisanzala, Kata ya Lundi, Wilaya ya Morogoro, mkoani Morogoro.
Akizungumza katika ziara hiyo, Dkt. Kiruswa ameipongeza kampuni hiyo kwa kufikia hatua ya kuanza uzalishaji wa madini mkakati kwa matumizi ya teknolojia ya kisasa duniani, huku akisisitiza umuhimu wa utunzaji wa mazingira sambamba na maendeleo ya kiuchumi.
“Nachukua fursa hii kuwapongeza kwa hatua mliyofikia ya kuanza uzalishaji wa madini haya muhimu katika teknolojia ya kisasa. Hata hivyo, ni muhimu kuhakikisha mnatunza mazingira ipasavyo na kuwasilisha mpango wa ulinzi wa mazingira kama inavyotakiwa kisheria,” amesema Dkt. Kiruswa.
Aidha, ameitaka kampuni hiyo kutunza kumbukumbu sahihi za mradi huo kwa lengo la kujenga uelewa wa thamani yake kwa Taifa, zikiwemo takwimu za uzalishaji, idadi ya ajira zilizotolewa pamoja na kiasi cha fedha kilichotumika katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya jamii (CSR).
Katika ziara hiyo, Dkt. Kiruswa pia ametembelea kiwanda cha Guanui Mining Investment Group Ltd kilichopo kijiji cha Mkuyuni, Wilaya ya Morogoro, ambapo ameipongeza kampuni hiyo kwa uwekezaji wake mkubwa unaochangia ukuaji wa uchumi, huku soko la bidhaa zake likiwa ndani na nje ya nchi.
Sambamba na hilo, Naibu Waziri amekutana na kuzungumza na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Adam Malima, ambaye ameahidi kuendelea kushirikiana kwa karibu na Wizara ya Madini pamoja na Ofisi ya Madini Mkoa wa Morogoro ili kuongeza ufanisi na udhibiti wa makusanyo ya maduhuli ya Serikali.
Kwa upande wake, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Morogoro, Zabibu Mapacho, amesema Ofisi ya Madini Morogoro inaendelea kushirikiana kwa karibu na Serikali za Manispaa, Wilaya na vijiji kwa lengo la kuongeza tija katika uzalishaji wa madini na upatikanaji wa taarifa sahihi za shughuli za sekta ya madini.
Naye, Meneja wa Kampuni ya Synergy Tanzania Company Ltd, Sanjay Dabhi, amesema kiwanda hicho kimeajiri wafanyakazi zaidi ya 120 wa kudumu na wafanyakazi 66 wa muda mfupi. Ameongeza kuwa kampuni hiyo inashiriki kikamilifu katika utekelezaji wa miradi ya uwajibikaji kwa jamii zinazozunguka eneo la mradi.
Awali, Dkt. Kiruswa alitembelea Ofisi ya Madini ya Mkoa wa Morogoro kwa lengo la kupata taarifa za kina kuhusu shughuli za madini katika mkoa huo, ambapo alipata pia fursa ya kuzungumza na watumishi wa ofisi ya madini wa mkoa huo.








