…..…………….
Jeshi la Polisi Tanzania linaendelea kuwekeza kikamilifu katika mafunzo ya ndani na nje ya nchi kwa maafisa, wakaguzi na askari wa vyeo mbalimbali, kwa lengo la kuboresha utendaji kazi na kuimarisha huduma bora kwa wananchi, hususan katika kulinda usalama wa maisha na mali zao.
Katika muktadha huo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe Kamishna Msadizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Augustino Senga,, tarehe 30 Desemba, 2025, alimshukuru Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP) Camillus Wambura kwa juhudi zake za kutafuta na kuwezesha nafasi za masomo kwa askari wa Jeshi la Polisi Nchini, hatua inayoongeza ujuzi na weledi katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku.
Shukrani hizo zimetolewa katika ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe iliyopo Vwawa Wilaya ya Mbozi kufuatia Mkoa wa Songwe kupata nafasi ya mafunzo ya kimataifa, ambapo Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Abednego Kiyenze, kutoka Kikosi cha Kutuliza Ghasia Mkoa wa Songwe, alichaguliwa kwenda kusoma nchini Cairo, Misri, katika Chuo cha taaluma ya Polisi na Kituo cha Utafiti (Police Academy, Research Center), akisomea Sayansi ya Polisi.
Mafunzo hayo yalishirikisha nchi 21 kutoka Bara la Afrika, ambapo Mkaguzi Msaidizi Abednego Kiyenze aliibuka mwanafunzi bora kwa kushika nafasi ya kwanza, akiongoza katika masomo ya darasani na ya nje ya vitendo na ukakamavu, ikiwa ni mafanikio makubwa yanayoitangaza vyema Tanzania na Jeshi la Polisi kwa ujumla.
Akizungumza katika tukio hilo, Kamanda Senga, alimpongeza Mkaguzi huyo kwa juhudi na nidhamu ya hali ya juu, na kumtaka kutumia elimu na uzoefu alioupata kuwanufaisha askari wengine wa Mkoa wa Songwe ili kuongeza ufanisi wa Jeshi kwa ujumla.
Aidha katila hatua nyingine, Kamanda Senga aliendelea kumuomba IGP Wambura kuendelea kutafuta nafasi zaidi za mafunzo ya ndani na nje ya nchi kwa askari wa Jeshi la Polisi, ili kuendana na mabadiliko ya kisayansi na kiteknolojia, na hivyo kuimarisha huduma kwa wananchi.
Kwa upande wake, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Abednego Kiyenze alimshukuru Kamanda Senga kwa kumuamini na kumteua miongoni mwa askari wengi, na kuahidi kuwa elimu na ujuzi alioupata nchini Misri atauitumia kwa weledi mkubwa, ikiwa ni pamoja na kuwafundisha askari wenzake pamoja na viongozi wake, ili kuongeza ufanisi katika majukumu ya kazi za kila siku.






