Tamasha linalosubiriwa kwa hamu la Samia Fashion Festival linatarajiwa kuzinduliwa, likiwaunganisha pamoja vipaji vikubwa vya mavazi vya Tanzania, magwiji wa sekta hiyo, na wahusika wa kitamaduni. Mkutano rasmi na waandishi wa habari umefanyika Ijumaa, 11 Oktoba 2024, katika Ukumbi Wa Serena, Jijini Dar es Salaam, ambapo maelezo ya tukio hilo yataelezwa.
Tamasha hili limepewa jina kwa heshima ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na limelenga kukuza utamaduni wa Tanzania kupitia mavazi huku likionyesha mchango wa Rais katika sekta ya ubunifu. Tamasha litaendelea kwa siku saba, likijumuisha matukio mbalimbali ya kuwawezesha wanawake, watoto, na vijana kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.
Kauli mbiu ya tamasha hili ni “Ubunifu na Stara”. kauli mbiu hii ni taswira tosha ya nafasi na haiba ya mama yetu mpendwa Dkt Samia Suluhu Hassan, na kwa. Jinsi gani jamii inaweza kutumia haiba hiyo yenye stara katika nyanja mbali mbali za kijamii, kama vile motiko, sherehe, shughuli za jioni, malezi, na kadhalika.
Shughuli muhimu zitakazosindikiza tamasha letu hili ni pamoja na:
- Siku ya Vipaji vya Mavazi Vinavyochipukia (27 Oktoba 2024): Shughuli hii itahusisha maonesho ya mavazi ya watoto (children na Young Adults)itakayolenga kuonesha vipaji vya watoto na vijana. Tukio hili litakuwa ni tukio la mchana litakaloongozwa na watoto na vijana vinara katika tasnia ya mavazi na ubunifu.
- Usaili wa Warembo: Shughuli hii itafanyika Dar es Salaam, na itaangazia wabunifu na warembo; lengo kuu likiwa kuchagua warembo wa kushiriki katika tamasha kuu.
- Siku ya Zanzibar (Zanzibar Day): Maonesho ya mavazi yatakayofanyika katika eneo la Ngome Kongwe, Zanzibar. Shughuli hii italenga kuadhimisha urithi wa kiutamaduni na ubunifu wa Zanzibar.
- Tukio Kuu la Tamasha (Grand Finale): Hili litafanyika Dar es Salaam, ambalo pia litawahusisha wadau mbali mbali, kutokea rika mbali mbali, yote katika lengo la kusherehekea ubunifu na stara katika fasheni.
“Tamasha hili si sherehe ya mavazi tu; ni jukwaa la kuonyesha ubunifu wa Kitanzania na ni heshima kwa uongozi na maono ya Mama Samia Suluhu Hassan,” alisema Khadija Mwanamboka, muandaaji wa Tamasha hilo.
Tamasha hili litafuatiliwa kupitia vyombo vya habari vya televisheni, redio, na mitandao ya kijamii, kuhakikisha ushiriki na mwitikio wa kitaifa.