Na. Dennis Gondwe, MWAJA, CHAMWINO
VIONGOZI bora wa serikali za mitaa wanachaguliwa na wananchi waliojiandikisha katika orodha ya wapiga kura ili waweze kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Kauli hiyo ilitolewa na mkazi wa Mtaa wa Mwaja, Kata ya Chamwino, Josephine Joseph alipoongea na mwandishi wa habari hii muda mfupi baada ya kujiandikisha katika orodha ya wapiga kura katika kituo cha Shule ya Msingi Chinangali.
Joseph alisema kuwa kujiandikisha ni haki yake na haki ya kila mwananchi mwenye sifa za kujiandikisha. “Viongozi bora wa serikali za mitaa wanachaguliwa na wananchi wenyewe.
Hivyo, ili uweze kumchagua kiongozi bora, sifa ya kwanza uwe umejiandikisha kwenye orodha ya wapiga kura katika mtaa wako. Bahati nzuri sifa ni za kawaida sana, kwamba awe na umri wa kuanzia miaka 18 na kuendelea, awe mtanzania mwenye akili timamu zaidi awe ni mkazi wa mtaa ambao uchaguzi unafanyika. Hii ni haki ya kila mtu mwenye sifa kujiandikisha na kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa” alisema Joseph.
Akiongelea tofauti ya zoezi lililopita la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura na orodha ya wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa alisema kuwa uboreshaji daftari la kudumu la wapiga kura ulilenga maandalizi ya uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani.
Orodha ya wapiga kura itahusu kumchagua mwenyekiti wa mtaa na halmashauri yake. Zoezi la uboreshaji daftari la kudumu la mpiga kura ulilenga kuboresha taarifa za watu waliohama toka sehemu moja kwenda nyingine, kupoteza kitambulisho cha mpira kura na kuandikisha watu waliofikisha miaka 18 ila orodha ya wapiga kura inahusisha wananchi wanaoishi katika mtaa husika, aliongeza.
Alisema kuwa viongozi wa serikali za mitaa ni muhimu sana katika jamii. “Viongozi hawa ndiyo wanaosaidia katika kuhamisisha shughuli za maendeleo na shughuli nyingine za kijamii kama usafi wa mazingira na utunzaji wa mazingira” alisema Joseph.
Mtaa wa Mwaja ni moja kati ya mitaa minne inayounda Kata ya Chamwino ukiwa na vituo vya kuandikisha wapiga kura vitatu.