Na Mwandishi wetu Michuzi Tv
KAMATI Tendaji ya Utekelezaji wa Mradi wa Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Kuimarisha Uangazi wa Hali ya Hewa (SOFF) umekutana kwa mara kwanza kwa lengo la kupitia na kuidhinisha nyaraka muhimu za kuanza rasmi utekelezaji wa Mradi huo nchini Tanzania.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao hicho, leo Oktoba 16,2024 katika Hotel ya Morena mkoani Morogoro, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC), Dkt. Ladislaus Chang’a amewashukuru wajumbe wa kamati tendaji kwa kukubali kuwa sehemu ya kusimamia utekelezaji wa Mradi wa SOFF Tanzania.
Aidha, Dkt. Chang’a ametoa shukrani zake za dhati kwa Sekretarieti ya SOFF na WMO kwa kuichagua Tanzania kuwa miongoni mwa wanufaika wa ufadhili wa fedha za Mfuko huo takribani dola za kimarekani milioni 9.
“Uwepo wenu ni ushahidi tosha wa dhamira yenu ya kusaidia kuboresha huduma za hali ya hewa kwa nchi yetu, kikanda na Duniani kote, huduma ambazo zitaenda kusaidia shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi”, amesema Dkt. Chang’a.
Aidha, Dkt. Chang’a ameongeza kuwa uanzishwaji wa mradi wa SOFF utasidia nchi kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa data za hali ya hewa na mfumo wa mawasiliano wa ubadilishanaji wa data hizo kimataifa kwa kuwezesha masuala ya muhimu ya kiufundi na kifedha.
Kwa upande wake, Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Shigeki Komatsubara ameeleza jinsi anavyoridhishwa na uongozi mzuri na utendaji kazi wa TMA na wataalamu wake kwa ujumla, na kuifanya Tanzania kuwa mfano wa kuigwa katika bara la Afrika.
Aidha, amesisitiza kuwa mradi wa SOFF utatoa msaada endelevu wa uendeshaji na matengenezo na usimamizi kwa vituo vya hali ya hewa vitakavyojengwa kuwa katika hali nzuri na endelevu kwa muda mrefu kwa kuwa UNDP imejipanga kikamilifu katika kufikia malengo na mafanikio hayo.
Naye Mwakilishi kutoka Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP), Clara Makenya ameendelea kusisitiza umuhimu mkubwa wa kuimarisha ushirikiano katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa na kuimarisha huduma za hali ya hewa.
Clara pia amefafanua jukumu la UNEP katika kufanikisha mradi huo, ikiwa ni pamoja na kusimamia viwango vya ubora katika utekelezaji wa mradi hususan eneo la mazingira kwa kuratibu na kutoa ushauri pale inapobidi kwa maendeleo endelevu ya nchi na dunia kwa ujumla.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC), Dkt. Ladislaus Chang’a akizungumza wakati wa kikao cha kamati tendaji ya Utekelezaji wa Mradi wa Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Kuimarisha Uangazi wa Hali ya Hewa (SOFF). Mkutano huo umefanyika leo Oktoba 16,2024 katika Hotel ya Morena Mkoani Morogoro.