Na Mwandishi wetu, Ngorongoro
Wananchi wapatao 56,000 katika Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro wanatarajiwa kufikiwa na Elimu ya Mpiga Kura kupitia juhudi za asasi za Haki Mwananchi na Mtanzania Foundation, asasi ambazo zimepewa kibali rasmi na Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kutoa elimu hiyo muhimu pamoja na kushiriki katika zoezi la Uangalizi wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika mwaka 2024.
Timu za asasi hizo zimewasili rasmi katika ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro na kujitambulisha kwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Bw. Benezeth Bwikizo, kuashiria kuanza rasmi kwa mchakato huo.
Elimu ya Mpiga Kura itatolewa katika kata zote 28 za Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro, ikilenga kufikia wananchi 56,000. Katika hatua za awali za utekelezaji, Mkurugenzi Mtendaji wa Haki Mwananchi na Mtanzania Foundation, Joseph Bahebe, alieleza kuwa asasi hizo zitatoa mafunzo maalum kwa watoa elimu watakaosaidia kusambaza Elimu ya Mpiga Kura. Mafunzo haya yatatolewa kupitia semina elekezi za siku mbili zitakazofanyika katika maeneo ya Loliondo, Sale, na Ngorongoro.
Semina ya kwanza inatarajiwa kufanyika siku ya Ijumaa, tarehe 25 Oktoba 2024, katika Tarafa za Loliondo na Sale, na semina ya pili itafanyika siku ya Jumamosi, tarehe 26 Oktoba 2024, katika Tarafa ya Ngorongoro. Lengo kuu ni kuhakikisha kuwa watoa elimu wote wanapata uelewa wa kina na mbinu bora za kuwafikia wananchi katika maeneo yao husika.
Kwa mujibu wa mpango huo, wakufunzi 17 kutoka kata 17 za Tarafa za Loliondo na Sale watashiriki semina hiyo ya kwanza, ilhali Tarafa ya Ngorongoro itakuwa na wakufunzi 11 kutoka kwenye kata 11 za eneo hilo, na hivyo kufanya jumla ya wakufunzi 28 watakaopewa jukumu la kusambaza Elimu ya Mpiga Kura. Kila mmoja wa wakufunzi hawa anatarajiwa kuwafikia wananchi takribani 200 ndani ya muda wa siku tano, kuanzia tarehe 26 Oktoba hadi 31 Oktoba 2024.
Kutokana na mpango huo, jumla ya wananchi 5,600 wanatarajiwa kufikiwa moja kwa moja na Elimu ya Mpiga Kura kupitia mafunzo ya wakufunzi hawa 28. Mbinu inayotumika ni kwamba kila mwananchi aliyepokea elimu hiyo ataombwa kuisambaza kwa wananchi wengine 10, hali itakayowezesha kufikia takribani wananchi 56,000 katika Halmashauri yote ya Wilaya ya Ngorongoro, ambayo ina jumla ya zaidi ya wananchi 120,000 walioandikishwa kupiga kura katika uchaguzi huo wa Serikali za Mitaa.
Mbali na kutoa elimu, Haki Mwananchi na Mtanzania Foundation pia zimepanga kushiriki kikamilifu katika zoezi la Uangalizi wa Uchaguzi. Uangalizi huu utahusisha kipindi chote cha kampeni za uchaguzi, kinachotarajiwa kuanza tarehe 20 Novemba na kuendelea hadi tarehe 26 Novemba 2024, na pia siku yenyewe ya uchaguzi itakayofanyika tarehe 27 Novemba 2024. Lengo ni kuhakikisha kuwa uchaguzi unafanyika kwa njia ya haki, huru, na uwazi.
Hii ni sehemu ya juhudi za muda mrefu za kuhakikisha kuwa wananchi wanapata uelewa wa kutosha kuhusu haki na wajibu wao katika michakato ya uchaguzi, sambamba na kuhakikisha kuwa zoezi la uchaguzi linazingatia viwango vya juu vya uadilifu na usimamizi bora.