Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ndg. Baraka Leonard amewataka Watumishi wa Ofisi ya Bunge kuendelea kufanya kazi kwa weledi na kwa kujituma huku wakizingatia kanuni na sheria za kazi.
Katibu wa Bunge ameyasema hayo leo tarehe 26 Oktoba, 2024 katika kikao kilichowakutanisha Watumishi wote wa Ofisi ya Bunge katika Ukumbi wa Pius Msekwa.
Katibu wa Bunge ambaye alikutana na Watumishi hao kwa mara ya kwanza tangu ateuliwa kushika wadhifa huo amesema ameelezwa kwamba Watumishi wa Ofisi ya Bunge wanafanya kazi kwa kujituma jambo ambalo pia yeye amelishuhudia.
“Nimeelezwa kwamba mnafanya kazi kwa kujituma na mimi nimeshuhudia hilo. Hongereni kwa hilo na naomba muendelee na ari hiyo ya kufanya kazi kwa kujituma,” aliongeza.
Katibu wa Bunge amewaeleza pia Watumishi hao matarajio yake kwao kwamba anatarajia waendelee kufanya kazi kwa ushirikiano, nidhamu, upendo na weledi wa hali ya juu.
“Kikao hiki ni muhimu kwangu ili niweze kuwaeleza yale nayotarajia kutoka kwenu na mimi niwaeleze ahadi zangu kwenu,” alisema.
Katibu wa Bunge aliwakumbusha Watumishi hao pia kwamba ushirikiano hauwezi kuwepo sehemu yenye majungu, fitina na ushirikina.
“Naamini katika kufanya kazi kwa ushirikiano. Nafananisha utendaji kazi na timu kama ya mpira, ushrikiano ndio hatimaye unaleta ushindi na watu wanashangilia. Ushirikiano hauwezi kujengwa sehemu yenye majungu. Taasisi yenye amani na upendo kazi inaenda vizuri,” alisema.
Katibu wa Bunge pia aliwaeleza Watumishi hao kwamba hatowaendekeza wala hatowavumilia wale wote wataokuwa wanafanya kazi kwa fitina, majungu, upendeleo na kwa kusababisha migawanyiko.
“Mfanye kazi kwa upendo na palipo na upendo hakuna fitina wala majungu. Sitoweza kuelewana na mtu anayependelea na anayegawanya watu,” alisema.
Mbali na hayo Katibu wa Bunge aliwaeleza Watumishi hao kwamba yeye ni mtu anayefikika na sikuzote milango yake itakuwa wazi kwa ajili ya kuzungumza na Watumishi au Mtumishi yoyote pale kutakapokuwa na changamoto yoyote ya kazi.
“Mimi nafikika kwa hiyo kama kuna tatizo nitafute kwenye simu au njoo Ofisini tuzungumze,” alisema.
Sambasamba na matarajio hayo Katibu wa Bunge amewaeleza Watumishi hao kwamba iwapo watafanya kazi kulingana matarajio yake ahadi yake kwao ni kutengeza mazingira wezeshi ya kufanya kazi.
“Haya ninayotarajia kutoka kwenu kama mtayazingatia ahadi yangu kwenu ni kujenga mazingira wezeshi ya kufanya kazi,” alisema.