Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa amesisitiza uungaji mkono usioyumba wa nchi yake na mshikamano na watu wa Palestina, ambao wanaendelea kuvumilia mateso makubwa kutokana na miongo kadhaa ya uvamizi haramu.
Katika hotuba yake wakati wa ufunguzi wa kikao cha bunge cha mwaka 2025 mjini Cape Town, Ramaphosa alisisitiza kuwa Afrika Kusini imetekeleza wajibu wake chini ya Mkataba wa Mauaji ya Kimbari kwa kufungua kesi dhidi ya Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ).
Kiongozi huyo wa Afrika Kusini alisisitiza dhamira kamili ya nchi yake kwa kanuni za Umoja wa Mataifa, ikiwa ni pamoja na wajibu kwa nchi zote wanachama kutatua mizozo ya kimataifa kwa njia za amani.
Afrika Kusini imekuwa mtetezi mkubwa wa haki za Wapalestina katika jukwaa la kimataifa, huku hatua yake ya kisheria katika mahakama ya ICJ ikivuta hisia za kimataifa kuhusu ukiukaji wa haki za binadamu unaofanywa na utawala wa Israel katika Palestina inayokaliwa kwa mabavu.
The post Rais wa Afrika Kusini athibitisha kuunga mkono Palestina katika hotuba yake bungeni first appeared on Millard Ayo.