Na Janeth Raphael MichuziTv -Dodoma
Dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kuwa kila nyumba, jengo, kiwanja, huduma, ofisi ama eneo la biashara linatambulika kwa Anwani ya Makazi. Anwani ya Makazi inaundwa na Namba ya Anwani maarufu kama namba ya nyumba, jina la barabara au Mtaa na Postikodi. Postikodi ama nchi zingine zinaita Zipcode ni utaalamu wa kugawa maeneo ili kurahisisha utambuzi.
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habar Jerry Slaa ameyazungumza hayo leo jijini Dodoma wakati akifungua wiki ya huduma za makazi ambapo amesema
kwa hapa Tanzanians mgawanyo huo umefanyika katika ngazi ya kata ambapo kila Kata ina Postikodi yake yenye tarakimu tano.
Slaa amesema Anwani za Makazi inarahisisha utoaji na upokeaji wa huduma mbalimbali ili kuchochea maendeleo ya Kiuchumi na kijamii hasa katika zama hizi ambazo Mapinduzi ya 4,5 na 6 ya viwanda yanategemea matumizi ya TEHAMA.na matumizi ya TEHAMA yanalazimu kuwa na mifumo ya utambuzi ndiyo sababu ya Serikali kuanzia mfumo huo.
“Utekelezaji wa Mfumo wa Anwani za Makazi ulianza mwaka 2010 na kwa mujibu wa Mpango wa utekelezaji ulitakiwa ukamilike mwaka 2015 hata hivyo, utekelezaji wake ulikuwa wa kasi ndogo ukilinganisha na matarijio, hali iliyosababishakuanzishwa kwa Operesheni maalumu iliyojulikana kama Operesheni Anwani za Makazi ambayo ilizinduliwa na Mheshimiwa Rais, wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 08 Februari, 2022, na Operesheni hiyo ilifanyika nchi nzima na kusimamiwa na wakuu wa mikoa Tanzania Bara na Zanzibar.” – Slaa
Aidha, ifahamike kuwa nchi nyingi hususan za Kiafirika zimeshindwa kufikia hatua hiyo ya utekelezaji wa Mfumo na zimeanza kuja kujifunza Tanzania.
Hata hivyo kufuatia utekelezaji wa Operesheni hiyo, Mfumo wa Anwani za Makazi umeanza kutumiwa na baadhi ya wananchi na taasisi katika kurahisisha utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku; na matunda ama manufaa ya Mfumo yameanza kuonekana ambapo huduma mbalimbali zinatolewa kupitia mfumo wa Anwani za Makazi kama vile barua ya utambulisho ya kidijitali; Navigation Services,kuonyesha mahali locations na elimu inaendelea kutolewa kuhamasisha matumizi hayo.
Kwa upande wake Naibu Waziri Nchi Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Festo Ndugange amesema Mfumo wa Anwani za Makazi ni nyenzo ya utambuzi ambayo inatambulisha wakazi na makazi na uwepo wa mfumo kwa upande wa OR-TAMISEMI ni nyenzo muhimu zaidi kwani kwa mujibu wa Sheria na Kanuni za Serikali za Mitaa, jukumu la kutoa majina ya mitaa lipo OR-TAMISEMI, ambapo utekelezaji wa mifumo hiyo inarahisisha utekelezaji wa jukumu la kutoa majina ya mitaa.
Ndugange amesema TAMISEMI ni mdau mkuu katika utekelezaji hususan kupitia kwa Watendaji wa Kata, Vijiji na Mitaa ambao wana wajibu wa kuwezesha uwekaji wa miundombinu; kuhuisha taarifa na kukusanya taarifa mpya, lakini pia TAMISEMI ni mnufaika mkubwa katika matumizi ya Mifumo hiyo ni kwa kuzingatia kwamba Mfumo unawezesha utambuzi hivyo hurahisisha utoaji na upokeaji wa huduma.
“Tamisemi ndiyo yenye wananchi na ndiyo mtoa huduma mkuu kwa wananchi, hivyo TAMISEMI inauhitaji sana Mfumo huu na kwa sasa tulifanya majaribio ya kutoa barua kwa njia ya kidijitali ambapo jambo hilo limeonyesha kuwa la mafanikio” – Ndugange
Aidha kwa upande wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na Ofisi ya Rais TAMISEMI Mchengerwa amesema wamekubaliana kuendelea kutoa Mafunzo ya Mfumo wa Anwani za makazi kwa Waratibu wa Mikoa na Halmashauri..
Mafunzo mengine yatakuwa yanatolewa kwa njia ya TEHAMA (online training), hivyo Makatibu Tawala wa Mikoa na Wakurugenzi wa Halmashauri wametakiwa waruhusu, kuwahamasishe na muwahimize Waratibu wao kushiriki mafunzo hayo kwa kadri ratiba zitakazoandaliwa.
“Tutaweka mazingira ya kutoa msaada wa kiufundi pale inapohitajika wakati wote. Hatua hizi ni kudhibiti changamoto kwa mwananchi kutokuwa ama kutotambua Anwani yake.”