Na Mwandishi Wetu,Unguja
MFUKO wa Maendeleo ya Jamii(TASAF) umetoa pongezi kwa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu nchini kwa kukubali ombi la kuwapatia mikopo wanafunzi wanaotoka kaya masikini wapate mikopo kwa asilimia kubwa
Pongezi hizo zimetolewa na Ofisa Ufuatiliaji kutoka TASAF Ramadhan Madari wakati wa Maonesho ya maadhimisho ya miaka 20 ya Bodi ya Mikopo yaliyofanyika hivi karibuni katika viwanja vya Kisonge Unguja visiwani Zanzibar.
Amesema wamefanikiwa kutoa mikopo kwa asilimia kubwa kwa wanafunzi wanaotoka katika kaya hizo ingawa bado wanaona hazitoshi na kufafanua kuwa ukienda vijijini wazee wanashindwa kumudu gharama hizo .
“Na wengine wanatoka kijijini unakuta mwanafunzi anapewa Sh.600,000 kwa muhula mmoja kwahiyo anatakiwa aongezee Sh.400,000 hawana uweze ni kaya masikini hali inakuwa ngumu.Kwahiyo ni kweli kama kuna uwezekano vijana hawa wapewe asilimia 100 ukizingatia wanatoka kwenye kaya masikini na ni kweli masikini hazina uwezo,” amesema
Katika kusisitiza hilo, Madari amesema “hii wiki ni ya mitihani, kwa siku mbili nyuma nimepokea maombi mengi ya wanafunzi wanataka tuwadhamini angalau wafanye mitihani familia zimekosa, bodi imelipia tayari lakini mzazi anashindwa kumalizia kinachobaki.”
Kwa upande wake Meneja Utawala Bodi ya Mikopo, Claud Casmir amekiri kuwpo na upungufu wa fedha licha ya wanuafaika wa Tasaf kupewa kipaumbele cha mikopo japo zinajitokeza changamoto za hapa na pele ikiwemo kiwango kidogo cha fedha.
“Bodi ya mikopo kuadhimisha miaka hii 20 lengo kubwa ni kuangalia namna gani tunaweza kupata vyanzo vingine vya fedha mfuko uweze kuwa mkubwa ili wenye mahitaji wapate, hata hawa wa Tasaf wapate asilimia asilimia 100,” amesema
Awali wanafunzi wanaopata mikopo kupitia TASAF wameiomba Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu Tanzania (HESLB) kuwapatia mikopo kwa asilimia 100 ili kumudu gharama mbalimbali zinazohitajika wakiwa vyuoni.
Rashid Ali Abdalla ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa kwanza Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (Suza) amesema alianza kunuafaika na TASAF akiwa darasa la tano mpaka sasa yupo chuoni.
“Tumepata mikopo kupitia kaya masikini, tumesaidika kwani wazazi wangu hawakuwa na uwezo wa kunisomesha,” amesema na kuongeza licha ya mchango huo kulingana na kiasi wanachokipata wanashindwa kumudu gharama zote za mahitaji na kuomba bodi iwaangalie kwa jicho la kipekee waweze kusoma bila changamoto.
Mwanafunzi Il-Kham Ali Abdalla wa mwaka wa kwanza fani ya Uhasibu na Fedha Suza, amesema wanashukuru kwa kupewa kipaumbele wanufaika wa Tasaf katika kupewa mikopo.”Tunaiomba Serikali kupitia bodi ya mikopo ituwekee angalau asilimia 100 kwasababu kile kiasi kinachobaki bado familia zetu hazimudu kulipa,” amesema Il-Kham ambaye anapata mkopo kwa asilimia 62.
Mwanafunzi mwingine Mtumwa Ali Hija kutoka shehia ya Chaani Masingini ambaye amenufaikaa na Tasaf tangu darasa la sita hadi sasa akiwa chuo kikuu, amesema kusingekuwa na mfuko huo asingesoma akikumbushia jinsi alipofaulu masomo ya kidato cha nne lakini wazazi wake wakamwambia atafute kazi ya kufanya maana hawana uwezo.