
Katibu wa Jukwaa la vijana ya ACTIVISTA Tanzania, Arif Fazel katikati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
JUKWAA la vijana ya ACTIVISTA Tanzania imetoa wito kwa serikali na wadau wa sekta ya nishati kuhakikisha sera zinazoongoza sekta hiyo ni jumuishi, endelevu, na zenye uwazi.
Wito huo umetolewa na mwishoni mwa wiki na Katibu wa Jukwa hilo, Arif Fazel kufuatia Mkutano wa Mission 300 Energy Summit uliofanyika jijini Dar es Salaam mwezi Januari, ambao ulilenga kuwaunganisha Waafrika milioni 300 na umeme ifikapo mwaka 2030.
“Vijana walikuwa na uwakilishi mdogo katika mkutano huo licha ya kuwa zaidi ya asilimia 60 ya idadi ya watu nchini Tanzania.”
Amesitiza kuwa vijana wanapaswa kushiriki kikamilifu katika mijadala na maamuzi yanayohusu nishati, kwa kuwa yanaathiri mustakabali wao moja kwa moja.
Aidha, jukwaa hilo imeeleza wasiwasi wake kuhusu msisitizo uliowekwa kwenye nishati za kisukuku (fossil fuels) katika ahadi za uwekezaji wa zaidi ya dola bilioni 5 zilizotolewa katika mkutano huo.
Ameeleza kuwa hatua hiyo inakinzana na jitihada za kimataifa za kupambana na mabadiliko ya tabianchi na inapunguza kasi ya Afrika katika kuhamia kwenye vyanzo vya nishati safi na endelevu kama vile jua, upepo, na jotoardhi.
Vilevile, Fazel amekosoa ukosefu wa uwazi katika mikataba ya nishati na miradi inayopangwa, ikisisitiza kuwa Watanzania wanastahili kufahamu jinsi rasilimali zao zinavyotumiwa.
Amesisitiza kuwa miradi ya nishati lazima iheshimu haki za binadamu, ilinde mazingira, na kuepuka kuwahamisha watu kwa nguvu.
Pia Fazel ametoa mapendekezo yafuatayo kwa Serikali ya Tanzania na wadau wa nishati,
Kuhakikisha ushiriki wa vijana, wanawake, na makundi yaliyotengwa katika uundaji wa sera na miradi ya nishati.
Kuongeza uwazi katika sekta ya nishati kwa kuweka wazi mikataba ya uwekezaji na tathmini za athari za mazingira.
Pia Kuhakikisha nishati inapatikana kwa bei nafuu na kwa usawa kwa makundi yote ya wananchi, hasa jamii zilizotengwa.
Kuimarisha usimamizi wa sekta ya nishati kwa kushirikisha vijana katika maamuzi na kutekeleza mifumo ya uangalizi huru.
Hata hivyo amesisitiza kuwa huu si wakati wa ahadi zisizotekelezwa bali ni wakati wa kuchukua hatua. Wamesema kuwa mpito wa Tanzania kuelekea nishati endelevu haupaswi kuwa fursa kwa wachache bali haki kwa kila Mtanzania.
“Pamoja, tuijenge Tanzania yenye nishati endelevu, jumuishi, na yenye haki kwa wote.”