Wananchi Mkoa wa Songwe wametakiwa kuhakikisha wanashiriki katika michezo mbalimbali ili waepukane na vitendo vya uhalifu ambavyo vinaweza kuleta madhara kwa jamii.
Hayo yalisemwa Februari 19, 2025 na Afisa Mnadhimu wa Polisi Mkoa wa Songwe Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Akama Shaaban wakati akifungua Mashindano ya Polisi Famili Day Cup ambayo yanafanyika katika Viwanja vya CCM Vwawa Wilaya ya Mbozi, yakiwa na kauli Mbiu isemayo “Ni Wajibu wa Polisi Kushirikiana na Jamii ili Kutokomeza Uhalifu”
Baada ya ufunguzi huo ACP Akama amesema kuwa michezo ni ajira pia inajenga afya ya akili na mwili hivyo amewataka Wananchi hao kutumia fursa ya michezo katika kuvumbua vipaji ambavyo vitakuwa fursa kwao na jamii zao ili kuendesha maisha yao ya kila siku na kujiepusha kutokufanya shughuli zisizohalali ikiwa ni pamoja na kujiingiza katika vitendo vya kihalifu.
Pamoja na mambo mengine ACP Akama amewataka wananchi hao pamoja na wana michezo wanaoshiriki ligi hiyo kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kuhakikisha wanatoa taarifa za uhalifu na wahalifu ikiwa ni pamoja na vitendo vya ukatili ili wahusika waweze kuchukuliwa hatua za kisheria haraka ikiwemo kufikishwa mahakamani.
Kwa upande wake, Mratibu wa Mashindano hayo Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) John Maro ambaye ni Mkuu wa Kituo cha Polisi Mlowo alitoa elimu kwa wananchi na washiriki wa ligi hiyo juu ya madhara ya kutokufanya mazoezi na kubainisha umuhimu na faida za michezo kwa maisha ya mwanadamu na kuwataka kutumia fursa hiyo kuwa chachu ya kuibua vipaji vyao katika jamii ambavyo vitaweza kuwasaidia katika nyanja mbalimbali za kukuza na kuutangaza mchezo wa mpira wa miguu ndani na nje ya Mkoa wa Songwe.
Mashindano hayo yanahusisha timu nane (8) ambapo katika hatua ya ufunguzi yamehusisha timu ya Magereza Fc na Mlowo United ambao Magereza Fc wameibuka washindi kwa kufunga magoli matatu kwa moja (3-1) dhidi ya mpinzani wake Mlowo Fc.