Na Mwandishi wetu, Pwani.
Shule ya Sekondari Baobab ipo Kata ya Mapinga, Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo Mkoani Pwani; mwaka huu inatimiza miaka ishirini huku ikiyataja baadhi ya mafanikio yake ndani ya kipindi hicho.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Bw. Venance Hongoa anayataja mafanikio hayo kuwa ni kuzalisha wataalam wa fani mbalimbali pamoja na kuendeleza vipaji vya wanafunzi wanaopitia shuleni hapo.
“Baadhi ya wahitimu wetu sasa ni wataalam katika fani mbalimbali walioko ndani na nje ya nchi yetu, “ anasema.
Bw. Hongoa anasema shule hiyo iliyoanzishwa rasmi Januari 2005 na kupewa namba ya Usajili S.1597 inamilikiwa na Asasi isiyo ya Kiserikali inayoitwa “SHAJAR SCHOOLS ASSOCIATION”
Anabainisha kuwa asasi hiyo imefanikiwa kuweka miundombinu bora na wezeshi kwa wanafunzi kujifunza na walimu kufundisha.
“Uwepo wa mazingira tulivu yenye maua na miti inayotoa hewa safi na viti maalum vya kujisomea maarufu kama “Vimbwete” umekuwa chachu ya wanafunzi wa shule hii kufanya vizuri Kitaaluma” anasema
Mwalimu Mkuu huyo anafafanua kuwa shule ina madarasa yenye hewa safi, Maabara za Sayansi zilizosheheni vifaa muhimu kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo, Vyumba vya kujifunza Kompyuta, Maktaba kubwa yenye vitabu muhimu, mabweni ya kisasa, viwanja vya michezo mbalimbali na Karakana (Workshops) kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo ya fani za ufundi.
Mafanikio ya Shule
Kuhusu Mafanikio; anasema kuwa mwaka huu 2025 shule inatimiza miaka 20 tangu ianzishwe. Katika kipindi hicho cha miaka ishirini, shule imejipatia mafanikio makubwa kitaaluma na kinidhamu. Miongoni mwa mafanikio hayo ni:
Shule imeweza kusimamia nidhamu ya wanafunzi, walimu na wafanyakazi mwega kwa kiwango cha hali ya juu. Nidhamu ndio kila kitu katika mafanikio ya Shule na hii imevutia wazazi / walezi wengi kuleta wanafunzi Shuleni Baobab.
Aidha, katika kipindi cha miaka 20, Shule inajivunia kuimarika kwa ufaulu wa wanafunzi katika Mitihani ya Taifa ya Kidato cha 2, 4 na 6 na hata kuweza kutoa wanafunzi bora Kitaifa kwa miaka mbalimbali. Alifafanua kuwa Baobab ni Shule inayodahili wanafunzi wenye ufaulu wa wastani wanaofundishika na kuwawekea mikakati madhubuti kisha kuhitimu Kidato cha 4 na 6 wakiwa na ufaulu bora hasa wa daraja la 1 na la 2. Alieleza kuwa zaidi ya asilimia 93 ya wahitimu wote wa Kidato cha 4 tangu 2008 hadi 2024 wamepata sifa za kujiunga na masomo ya Kidato cha tano na Vyuo vya kati. Kwa upande wa wahitimu wa Kidato cha 6, zaidi ya 97% wamepata sifa za kujiunga na Vyuo Vikuu ndani na nje ya nchi.
Alitaja baadhi ya mikakati wanayotumia kuimarisha ufaulu kuwa ni kuwapeleka wanafunzi kwenye Ziara za kimasomo ndani na nje ya Nchi ili kujifunza kwa vitendo yale waliyofundishwa kwa nadharia darasani. Baadhi ya maeneo waliyotembelea katika kipindi cha miaka 20 ni: Zanzibar, Bagamoyo, Mji wa Kilwa, Arusha, Dodoma, Kilimanjaro, Morogoro, Tanga, Mbuga za wanyama zilizomo Mkoani Arusha, Pwani, Morogoro na Iringa. Pia walitembelya Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Makumbusho ya Taifa, Hospitali ya Muhimbili na Ocean Road. Aidha, kwa ziara za nje ya nchi, wanafunzi wametembelea Shule rafiki iitwayo VIVA College iliyopo Jinja nchini Uganda mwaka 2017, 2018 na 2019.
Anayataja mafanikio mengine kuwa ni kuanzishwa kwa Mkondo wa Elimu ya Amali. Shule ya Sekondari Baobab ni miongoni mwa Shule chache zinazofundisha mafunzo ya fani za ufundi. Amezitaja baadhi ya fani zinazofundishwa kwa sasa kuwa ni: Electrical installation, Solar Power Installation, Motor Vehicle Mechanics, Food Production, Plumbing and Pipe fitting, Design, Sewing and Cloth Technology, Masonry and Bricklaying, Graphic Designs, Welding and Fabrications na Football. Katika fani zote hizi, mafunzo hutolewa kwa nadharia na vitendo.
Anaendelea kueleza kuwa fanikio jingine ni matumizi ya nishati safi ya “Bio gas” katika kupikia na hivyo kuhifadhi mazingira. Nishati hii hutumia mabaki ya vyakula na kinyesi cha binadamu na mifugo na hivyo imekuwa chachu katika kuweka mazingira ya Shule kuwa safi.
Katika kipindi tajwa pia Shule imefanikiwa kuboresha viwanja vya michezo. Shule imekuwa ikiboresha viwanja hivi ili viendane na viwango vya Kimataifa. Wanafunzi hushiriki kwenye michezo kulingana na ratiba iliyowekwa ili kuimarisha afya zao na kuwapatia ukakamavu.
Aidha, Baobab ni miongoni mwa Shule chache nchini zinazofundisha somo la Lugha ya Kichina. Ufundishaji wa somo hili umewasaidia wanafunzi kwani wanapohitimu masomo, wamekuwa na ushindani mkubwa Kimataifa katika soko la ajira kutokana na kuifahamu vema lugha ya Kichina ambayo huwapatia faida ya ziada yaani “Added Advantage” kwenye usaili.
Utekelezaji wa Sera ya Elimu ya mwaka 2014 – Toleo la 2023
Mkuu wa Shule anasema shule iko katika utekelezaji wa Sera tajwa ya elimu. Katika kutekeleza sera hiyo, Shule imeanzisha mafunzo ya elimu ya Ufundi, ambapo mwanafunzi huchagua fani mahususi moja kutegemeana na matakwa yake, uwezo wake na malengo yake kimaisha. Menejimenti ya Shule imejenga Karakana (Workshops) kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo ya fani za ufundi.
“Wanafunzi wa Baobab wanayo fursa ya kuchagua fani ya ufundi mojawapo wanayoipenda itakayowawezesha ama kuajiriwa au kujiajiri mara baada ya kuhitimu elimu ya Sekondari,” anasema Bw. Hongoa
Wanafunzi wa fani ya “Electrical Installation” wakifanya mafunzo kwa vitendo Shuleni Baobab
wanafunzi wavulana
sehemu ya wanafunzi wasichana